Huku Serikali ikikanusha kuhusika katika mauaji ya kiongozi wa upinzani wa Burundi, baadhi ya makundi ya kisiasa yameanza kuingiwa na wasiwasi kuhusiana na hatima ya kisiasa ya nchi hiyo, wiki moja baada ya Rais Pierre Nkurunziza kusogeza mbele tarehe uchaguzi wa wabunge.
Aliyeuawa ni Zedi Feruzi, aliyekuwa mkuu wa Chama
cha Umoja wa Amani na Demokrasia (UPD). Aliuawa mwishoni mwa wiki kwa
kupigwa risasi na watu wasiojulikana wakati akiwa nyumbani kwake.
Mauaji ya kiongozi huyo aliyeuawa pamoja na mlinzi
wake, yamechochea hisia za mgawanyiko miongoni mwa wanasiasa ambao
wanaendesha shinikizo kumtaka Rais Nkurunziza kutowania muhula mwingine
wa tatu wa uongozi.
Mwili wa Feruzi ulipatikana nje ya nyumba yake
huku watu walioshuhudia wakisema walisikia milio 20 ya risasi kabla ya
wahusika wa shambulizi hilo kutoweka kwa gari maalumu waliokuwa
wakitumia.
Kiongozi mwandamizi wa upinzani, Agathon Rwasa
alisema kuwa hakuna taarifa rasmi kuhusu ni nani aliyetekeleza mauaji
hayo ingawa alisema kuwa mwanasiasa huyo alikuwa mstari wa mbele kupinga
mkakati wa Rais Nkurunziza kuwania urais kwa muhula wa tatu.
Baada ya Feruzi kuuawa, vijana wa eneo hilo
waliandamana na kufunga barabara za mtaa huo kama sehemu ya kuonyesha
kutoridhishwa kwao na tukio hilo.
Kumekuwa na mfululizo wa matukio yanayohatarisha usalama na mshikamano wa taifa ikiwamo maandamano yanayoendelea kushuhudiwa kupinga hatua ya Rais Nkurunziza kuongeza muda wa kutaka kutawala.
Kumekuwa na mfululizo wa matukio yanayohatarisha usalama na mshikamano wa taifa ikiwamo maandamano yanayoendelea kushuhudiwa kupinga hatua ya Rais Nkurunziza kuongeza muda wa kutaka kutawala.
Zaidi ya watu 20 wamepoteza maisha tangu kuanza kwa vuguvugu la maandamano mwishoni mwa mwezi uliopita.
Shambulio la mwanasiasa huyo limetokea siku moja
baada ya shambulizi la bomu katika soko moja mjini Bujumbura
lililosababisha mauaji ya watu watatu na wengine takriban 40 kujeruhiwa.
“Tulisikia milio takriban 20 ya risasi, kila mtu
akalala chini, watu waliona gari aina ya Toyota likiondoka kwa kasi,”
alisema mkazi wa Ngagara ambaye hata hivyo, hakushuhudia mauaji ya
Feruzi.
Katika shambulio hilo, ofisa aliyekuwa miongoni
mwa waliopewa jukumu la kumlinda kiongozi huyo wa upinzani, alipata
majeraha mabaya.
“Tulikuwa tunarejea kwa miguu wakati gari aina ya
Toyota liliposimama karibu na sisi na wanaume waliokuwa ndani kuanza
kutufyatulia risasi,” alisema ofisa mwingine ambaye hakutaja jina lake.
Serikali yakanusha
Serikali imekanusha mara moja kuhusika na tukio hilo huku
ikisema imeshitushwa na mauaji hayo na kuongeza kuwa kisa hicho
kinapaswa kuchunguzwa mara moja ili waliolitekeleza unyama huo
wakabiliwe na mkono wa sheria.
Polisi imesema inamhoji mtuhumiwa wa shambulio hilo huku ikiwalaumu waandamanaji wanaoipinga serikali kwa kulitekeleza.
Huku hayo yakiarifiwa ,kiongozi wa mashirika ya
kiraia, Vital Nshimirimana ametupilia mbali madai ya polisi na kutoa
wito kwa jamii ya kimataifa kuchunguza kisa hicho.
“Hatujahusika kwa aina yoyote na shambulizi hili,
polisi wanajaribu kutupaka matope ili wapate sababu ya kuhalalisha
mauaji ya waandamanaji,” alisema Nshimirimana.
Majadiliano ya amani yaendelea kwa siri
Katika hatua nyingine, kumekuwa na ripoti juu ya
kuanza kwa mazungumzo yanayohusisha pande mbalimbali kwa ajili ya
kumaliza mzozo uliojitokeza katika siku za hivi karibuni ambao
unahatarisha umoja wa kitaifa.
Majadiliano hayo yanayoungwa mkono na jumuiya za
kimataifa ikiwamo mataifa jirani, yanaongozwa na Mwakilishi Maalumu wa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Maziwa Makuu, Said
Djintit.
Wengi wanaamini kuwa majadiliano hayo huenda
yakasaidia kutuliza mvutano wa kisaisa unaoendelea ambao umesababisha
maelfu ya raia kukimbia nchi za jirani za Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasi
ya Kongo (DRC) na Tanzania.
Mgogoro wa kisiasa nchini Burundi ulianza mwishoni
mwa Aprili baada ya chama tawala cha CNDD FDD kumteua Rais Nkurunziza
kugombea tena katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Juni 26.
Mzozo huo ulipanuka zaidi wiki iliopita baada ya
Jenerali wa Jeshi, Godefroid Niyombare kutangaza mapinduzi yalioshindwa
dhidi ya Serikali ya Nkurunzinza. Kutokana na hali hiyo uchaguzi wa
Bunge uliotarajiwa kufanyika Mei 26 umesogezwa mbele na sasa utafanyika
Juni 5.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia
Wakimbizi(UNHCR) limeelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa idadi ya
wakimbizi kutokana na ghasia zinazoendelea. Zaidi ya wakimbizi 50,000
wanaripotiwa kuingia nchini tangu kuanza kwa maandamano mwezi uliopita.
0 comments:
Post a Comment