Pages

Ads 468x60px

Wednesday, May 27, 2015

Wanasiasa wapigwe Marufuku kuingilia Sekta ya Elimu ili Sera Mpya ya Elimu ilete Tija


HIVI karibuni, Rais Jakaya Kikwete alizindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya Mwaka 2014, ambayo inaweka dira ya elimu na mafunzo nchini inayolenga kumfanya kila Mtanzania kuelimika kwa kupata maarifa, stadi za kazi, umahiri, uwezo na mitazamo chanya ili kuweza kuchangia katika kuleta maendeleo ya Taifa lao.

Dhima ya Sera hiyo ni kuinua ubora wa elimu na mafunzo na kuweka mifumo na taratibu zitakazowezesha kupata idadi kubwa ya Watanzania walioelimika na wanaopenda kujielimisha zaidi ili waweze kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa.

Hata hivyo, nionavyo mimi, sera hii mpya itakumbana na changamoto nyingi katika utekelezaji wake kutokana na mfumo mbovu wa elimu uliopo ambapo wahitimu katika vyuo vikuu vyetu nchini, mawazo yao ni kuajiriwa tu badala ya kujiajiri. 


Hadi sasa, kwa mtazamo wangu, mfumo wetu wa elimu unakosa vitu vitatu muhimu vinavyotakiwa kuwepo, ambavyo ni Maarifa, Kujenga stadi ya ujuzi na Elimu ya mtazamo wa kifikra.

Mambo hayo matatu yanamwezesha mwanafunzi anayehitimu masomo yake kwa mfano ya chuo kikuu kuwa na ujuzi na stadi za ufundi, unaotokana na asilimia 75 ya muda wake wa mafunzo kutengwa kwa ajili ya elimu ya vitendo. Mfano mdogo ni ule wa hivi karibuni, wa Serikali, kupitia Idara ya Uhamiaji, kutangaza kuwepo kwa nafasi za kazi 70 tu, lakini idadi ya vijana waliojitokeza kwenye usaili ili kupata nafasi hizo walikuwa zaidi ya 10,000.

Fikiria kila mwaka kuna maelfu ya vijana wanaohitimu vyuo vikuu lakini hawana ajira yoyote licha ya kuwa na vyeti vya kuhitimu kwa sababu tu wanasubiri kuajiriwa. Mawazo au fikra hizi za vijana wetu kusubiri kuajiriwa badala ya kujiajiri wenyewe na kuwaajiri wengine, ni tatizo la kimfumo. 

Serikali na taasisi zake, wanazo ajira ngapi kila mwaka ikilinganishwa na maelfu hayo ya wahitimu wa kila mwaka? Kimsingi, tatizo hilo la mfumo wetu wa elimu ndilo linalochangia kwa wasomi wetu washindwe kushindana katika soko la ajira la kimataifa, kwa kuwa huko wanakwenda kushindana na wasomi wa nchi nyingine zenye mfumo mzuri wa elimu unaozingatia maarifa na vitendo. 

Kwa hiyo basi, kama kweli tunataka kama taifa sera mpya hiyo ya elimu iweze kutekelezwa kwa vitendo, lazima wanasiasa waache kuingiza siasa katika mfumo wetu wa elimu, na badala yake wawaache wataalamu wa elimu ambao wamesomea na wanaielewa vilivyo sekta hiyo adimu kwa maendeleo ya Taifa, ndiyo wawe washauri wakuu wa Serikali. 

Haiwezekani Rais amteue Waziri wa Elimu asiyejua chochote kuhusu sekta ya elimu, halafu sisi kama taifa tutarajie kupata Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika Sekta ya Elimu! Sana sana, kitakachotokea ni BRN ya kisiasa ambayo itaonyesha wanafunzi kupata alama nzuri katika vyeti vyao, lakini katika hali halisi, wahitimu wote hao hawana ujuzi na maarifa, hivyo kuingiza nchi katika umasikini zaidi. 

Kwa vyovyote vile iwavyo, hata kama Serikali itaweka sera nzuri vipi katika sekta yetu ya elimu, endapo wanasiasa wataendelea kuingilia masuala muhimu yanayohusu elimu na kuingilia mambo ya kitaalam, itakuwa sawa na bure.

Kabla ya kuzinduliwa kwa sera mpya hiyo, mfumo wetu wa elimu umekuwa ukitekelezwa kwa kuzingatia sera mbalimbali, ikiwemo Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995, Sera ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya mwaka 1996, Sera ya Taifa ya Elimu ya Juu ya mwaka 1999 na Sera ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa Elimu Msingi ya mwaka 2007. 

Zamani, enzi za utawala wa awamu ya kwanza, wanafunzi wa madarasa la kwanza na la pili, walikuwa wanafundishwa masomo matatu tu ya Kusoma, Kuandika na Kuhesabu. Lakini tawala nyingine zilizofuata, zikavuruga mfumo huo na kuagiza wanafunzi wa ngazi hiyo kufundishwa masomo yote saba, sawa na wanafunzi wa darasa la tatu hadi la saba. 

Matokeo ya mabadiliko hayo, kila Mtanzania anayefuatilia mambo yanayojiri katika sekta hiyo ya elimu anayajua. Ni ongezeko la idadi ya wanafunzi wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu, ni miongoni mwao hao waliweza kuchaguliwa hata kuingia sekondari. Waliwezaje kufaulu, hadi kuchaguliwa kuingia sekondari, Serikali inajua. 

Kwa mujibu wa takwimu zinazotokana na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012, jumla ya Watanzania takriban milioni 11, walikuwa hawajui kusoma na kuandika. Hali hiyo, ndiyo imeilazimisha Serikali, katika kipindi chake hiki cha mwisho cha utawala, kurejesha tena mfumo ule wa zamani wa enzi za Mwalimu wa kufundisha masomo matatu ya Kusoma, Kuandika na Kuhesabu kwa wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili. 

Kwangu mimi, kutumba huko kwa mara kwa mara kwa elimu yetu nchini kutegemeana na mtawala aliyopo, kunatokana na kukosekana kwa mfumo bora wa elimu unaokubalika kwa makundi yote ya kijamii, yote hiyo ikiwa imechangiwa zaidi na wanasiasa wetu. Vitabu vilivyokuwa bora kwa kila ngazi ya elimu, waliviondoa na kuweka vya kwao kwa sababu tu za kisiasa na kiuchumi, kiasi cha kuwafanya wanafunzi wa darasa moja wa shule mbili tofauti kuwa na uelewa tofauti wa tafsiri au maana, kwa mfano ya somo la Jiografia au somo la Kemia.

0 comments:

Post a Comment

SHARE