WAZIRI wa Uchukuzi, Samuel Sitta ametangaza rasmi nia ya kugombea
urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM na kusema ana ari,
uwezo na utayari wa kuiimarisha nchi na kwamba kipindi kimoja tu cha
miaka mitano kinamtosha.
Mbali na hilo, Sitta amesema akifanikiwa kupata nafasi ya kuongoza
nchi atahakikisha anatenganisha masuala ya siasa na biashara, kwa sababu
ndiyo chanzo cha rushwa kubwa na kufikiwa kwa mikataba mibovu.
Alitangaza nia yake hiyo jana kwenye eneo la Itetemia (Ikulu) mkoani
Tabora ambako kulikuwa na makao makuu ya mashujaa wa Unyanyembe wakiwemo
Isike na Kiyungi walioendesha harakati dhidi ya dhuluma na unyanyasaji
wa wakoloni.
Pia, neno ‘Ikulu’ asili yake ni Itetemia baada ya Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere ilipofika mwaka 1961 kuamua kulitumia neno hilo
la Kinyamwezi liwe mbadala wa maneno ya kikoloni ya ‘State House’ kwa
ofisi na makazi ya mkuu wa nchi ambayo kwa sasa yapo eneo la Magogoni,
Dar es Salaam.
“Uimara wangu kiuongozi nitajumuisha nguvu na maarifa ya wananchi ili
tuvuke salama na pia tutekeleze kazi za maendeleo kwa ufanisi na tija
zaidi. ...nakuja kwenu Watanzania kuomba niwatumikie katika nafasi hii
ya juu ya uongozi. Ninayo ari, ninao uwezo na utayari wa kuiimarisha
nchi yetu katika kipindi cha miaka mitano ijayo ya utawala,” alisema
Sitta.
Katika hotuba yake hiyo, Sitta aliainisha baadhi ya vipaumbele na
kuwa kimojawapo ni kupambana kwa nguvu zote na vitendo vya rushwa kiasi
kwamba akifanikiwa kuingia madarakani atatenganisha masuala ya siasa na
biashara.
Akifafanua kuhusu hilo, Sitta ambaye aliwahi kuwa Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alisema rushwa kubwa zimekuwa na athari
mbaya kwa uchumi wa nchi yetu ambapo mikataba mibovu ya huduma na mauzo,
manunuzi hewa, manunuzi yaliyojaa unyonyaji, uteuzi wa wazabuni kwa
rushwa na hata rushwa katika ajira, vimesababisha hasara ya matrilioni
ya fedha kwa taifa.
“Uchumi unakosa afya kutokana na kubanwa na rushwa ambayo sasa
imeenea mijini na hata vijijini...kwa hatua ya kwanza hatuna budi
kutenganisha biashara na uongozi.
"Mtu achague kimoja; biashara au uongozi wa siasa. Ikiwa
mfanyabiashara atataka kuingia katika uongozi wa siasa itabidi akabidhi
mali na biashara zake kwa mdhamini atakayeendesha biashara hizo wakati
mhusika anatumikia Umma,” alisema Sitta.
Aliongeza kuwa kwa sasa baadhi ya wanasiasa na watumishi waandamizi
serikalini wanatumia nafasi zao kujitajirisha kupitia kujipendelea na
kuwa jambo hilo lina athari zake ikiwemo; kuchochea rushwa na usumbufu
kwa wananchi; kupunguza ari ya wafanyabiashara wa dhati na kudumaza
uwekezaji.
Sitta alitaja hatua nyingine katika kukabiliana na rushwa kuwa ni
kutunga sheria mpya zilizo kali na ambazo zitakuwa na matokeo ya kumzuia
mtu asitamani kusaka rushwa, mali za viongozi zitamkwe kwa uwazi, mali
isiyolingana na kipato na kukosa maelezo ya kutosheleza itaifishwe, kesi
za rushwa ziwe na utaratibu wenye uwazi na tume inayoshughulikia
maadili ya viongozi ipewe nguvu kubwa za uchunguzi na ufuatiliaji wa
mali za viongozi bila kuzuiwa na mamlaka yeyote.
“Sambamba na kupiga vita rushwa, hatuna budi kuchukua hatua kali
dhidi ya hujuma za uporaji wa maliasili za nchi na rasilimali zake.
"Madini, misitu, vyanzo vya maji, bahari, maziwa namito ni rasilimali
ambazo zisipotunzwa zitatishia uendelevu wa uchumi kwa vizazi vijavyo,
kwa hivyo uhalifu dhidi ya maliasili na rasilimali za nchi itabidi
uwekewe sheria na taratibu kali,” alionya Sitta.
Akieleza kuhusu vipaumbele vyake vingine, Sitta alisema kwa maoni
yake kipindi cha miaka mitano ijayo kina mwelekeo wa mifarakano katika
masuala ya Muungano, kutetereka kwa mshikamano kunakotokana na
chokochoko za siasa za ushindani, udini na kupanuka kwa tofauti ya
kipato na ongezeko la kundi kubwa hususani la vijana mijini lisilo na
uhakika wa ajira.
Kutokana na hali hiyo, alisema atatumia mchanganyiko wa uzoefu wa
uongozi kutanzua changamoto hizo ikiwemo ya Muungano. Kuhusu hilo la
Muungano alisema kwa sasa zinajitokeza kauli na vitendo ambavyo
vinaashiria kutaka nchi mbili zilizoungana zitengane.
“Kutoka Zanzibar, tunashuhudia wanasiasa wanaodai kuwa Zanzibar
itanufaika zaidi ikirejea kuwa na uhuru kamili bila kuwa ni sehemu ya
Muungano.
"Baadhi ya wabara nao wanawatazama ndugu zao wa Zanzibar kuwa ni
wakorofi wasioridhika na chochote kitakachofanywa na Muungano na
wanahisi kuwa mfumo wa Muungano uliopo unaipendelea Zanzibar ili hali
baadhi ya Wazanzibari nao wanadai kuwa Bara inapendelewa.”
Sitta alijinadi kuwa kiongozi anayeweza kuzileta pamoja kambi hizi na
kuuokoa Muungano hana budi kuwa na ufahamu mzuri wa kutosha wa asili,
misingi na manufaa ya Muungano.
“Ushiriki wangu katika serikali yetu tangu awamu ya kwanza ya uongozi
wa nchi yetu unaniweka katika nafasi nzuri ya kuongoza mchakato
utakaowezesha kuzijadili na kuzipatia ufumbuzi changamoto za Muungano.”
Kipaumbele kingine alitaja ni kuhusu mchakato wa Katiba ambapo
alisema licha ya mwafaka kamili kuhusu katiba mpya kutofikiwa, lakini
Katiba Inayopendekezwa ina maeneo mengi ya msingi ambayo yanaweza
kutuleta karibu ikiwa ni hatua ya awali inayowezesha kusonga mbele kwa
amani.
Jingine atakalolipa kipaumbele ni kujenga mfumo wenye motisha kwa
wote ili kuchochea uchumi endelevu na wa viwanda kukuza uchumi wa nchi
kwa kasi inayopunguza umasikini kwa haraka.
Aliongeza kuwa wafanyabiashara wakubwa wa ndani hawawekezi vya
kutosha ndani ya nchi ili kuleta maendeleo ya haraka ya huduma, viwanda,
kilimo na biashara na kuwa baadhi yao baada ya kuchuma fedha
wanazihamishia nje ya nchi huku watendaji serikalini wakiwatazama
wafanyabiashara hawa kuwa hawana uzalendo na ni wakwepa kodi na wana
mazoea ya kutoa rushwa.
Sitta anakuwa mwanasiasa wa kumi kutangaza nia ya kuwania urais huku
baadhi yao wameshachukua fomu za kuwania urais kwa tiketi ya CCM.
Waliotangaza nia na kuchukua fomu ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa, Waziri wa Kilimo, Chakula la Ushirika, Stephen Wassira, Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, Mbunge wa
Afrika Mashariki, Charles Makongoro Nyerere na mwanadiplomasia mkongwe
ambaye kwa sasa ni Balozi wa Umoja wa Afrika (AU) katika Marekani, Amina
Salum Ali.
Wengine waliotangaza nia ni Balozi mstaafu, Ali Karume, Waziri Mkuu
mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri wa zamani wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Waziri
wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani, Waziri wa Maliasili
na Utalii, Lazaro Nyalandu na Mbunge wa Nzega, Dk Hamisi Kigwangallah.
0 comments:
Post a Comment