Shule yafungwa kwa hofu ya simba mla watu
Mpekuzi blog
SHULE ya Msingi Saadani Chumvi iliyopo Kata ya Mkange wilayani
Bagamoyo mkoani Pwani, imefungwa baada ya wazazi kuwa na hofu baada ya
watu wawili na mbuzi 70 kuliwa na Simba kutoka kwenye Hifadhi ya Taifa
ya Saadani.
Shule hiyo ambayo iko jirani na hifadhi hiyo ilifungwa mwishoni mwa
mwaka jana kutokana na matukio hayo hali ambayo ilisababisha wazazi
kuogopa watoto wao kudhuriwa na wanyama hao hivyo kuwahamishia watoto
wao kwenye shule ya Msingi ya Saadani.
Akizungumza jana, Mtendaji wa Kijiji cha Saadani, Hussein Msilu
alisema mara baada ya matukio hayo wazazi wa watoto hao waliingia hofu
na kuwaondoa watoto wao wapatao 67 na kuwahamishia kwenye shule hiyo ya
Saadani ambayo iko umbali wa kilomita kati ya sita na saba.
Msilu alisema kutokana na hali hiyo uongozi wa kata na kamati ya
shule kwa pamoja walikubaliana wanafunzi hao kuhamishiwa kwenye Shule ya
Msingi Saadani kutokana na hofu iliyotanda kuwa wanafunzi wanaweza
kuliwa na simba hao.
Alisema wanaushukuru uongozi wa kiwanda cha chumvi kwa kutoa usafiri
kwa ajili ya kuwasafirisha wanafunzi kwenda na kurudi kutoka kwenye
Kitongoji hicho cha Saadani Chumvi hadi shuleni Saadani, kwani umbali
ulikuwa mrefu sana pia ni hatari kwani wanapita ndani ya hifadhi hiyo
ambayo ina wanyama mbalimbali.
Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete alisema alipata
taarifa hiyo na kuwasiliana na mamlaka husika na kwamba tayari
zilichukuliwa za kuwaondoa simba hao, lakini kilichobaki kwa sasa ni
hofu ya wananchi.
Aidha, aliwatoa hofu wazazi na kuwaambia wawarejeshe watoto hao
shuleni hapo ili waendelee kusoma hapo kwani ni karibu na makazi yao
tofauti na Saadani ambako ni mbali pia ni usumbufu mkubwa kwao, kwani
hali hiyo imedhibitiwa.
0 comments:
Post a Comment