Pages

Ads 468x60px

Sunday, June 21, 2015

Wananchi Wafunga Zahanati>>



WANANCHI wa Kijiji cha Ibondo Kata ya Katoro Wilaya ya Geita, wameifunga zahanati ya kijijini hapo kwa madai kuwa inatoa huduma mbovu licha ya kutoza wagonjwa fedha.
 
Tukio hilo lilitokea jana ambapo baadhi ya wananchi waliozungumza na Mpekuzi walieleza kuwa wanataka mganga mkuu na muuguzi wa zahanati hiyo waondolewe kwa sababu wameshindwa kutekeleza majukumu yao ya kazi.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, uamuzi wa kuifunga zahanati hiyo umefikiwa kwa sababu badala ya kutoa huduma inasababisha adha kwa wagonjwa.
 
Walisema walikwishafikisha malalamiko yao kwa mganga mkuu wa zahanati hiyo kuhusu utendaji mbovu wa muuguzi, lakini amekuwa akimkingia kifua.
 
“Kweli sisi kama wananchi wa Kijiji cha Ibondo tumechoshwa na mganga na muuguzi wa zahanati hii, wagonjwa wamekuwa wakinyanyaswa sana, tunatozwa fedha, unapokuwa hauna fedha unaambiwa ulete kuku, bata au mbuzi, mimi ni miongoni mwa watu tulioombwa rushwa ya kuku na wanapikiwa hapa hapa kituoni na manyoa ya kuku yapo,” alisema Juakali Daudi.
 
Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Mzee Kelomba mwenye umri wa miaka 70 alisema: “Rushwa… rushwa imefanya wananchi wa Ibondo tupate shida, huna pesa hakuna huduma. Lakini kama una chochote matibabu utapata, tena haraka.
 
“Nilimleta mjukuu wangu hapa apatiwe matibabu, lakini nilitazamwa kama sanamu mpaka nikampeleka kwa waganga wa kienyeji, matibabu kwa wazee ni tete tunahangaishwa sana.”
 
 Muda mfupi baadaye, askari wa kituo kidogo cha polisi cha Katoro walifika na kuvunja kufuli lililokuwa limewekwa na wananchi.
 
Pia walimkamata Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Lubadisha Sindano anayedaiwa kuhamasisha wananchi kuvamia zahanati na kuifunga.
 
Akijibu tuhuma za kupokea rushwa na kutoa huduma mbovu, muuguzi Justina Joseph, alisema kuwa tuhuma hizo si za kweli na kwamba mgogoro uliopo ni chuki za watu binafisi zinazosababishwa na masuala ya kisiasa.
 
Naye Mganga wa Zahanati hiyo, Asteria Nshekinabo, alikiri kufungwa kwa kituo hicho huku akitolea ufafanuzi suala la kutozwa fedha wagonjwa ambapo alisema wanaotozwa pesa ni wale ambao hawajajiunga na Mfuko wa Bima ya Afya (CHF).

0 comments:

Post a Comment

SHARE