WAZIRI
wa Nishati na Madini, George Simbachawene, amepata wakati mgumu
bungeni, kutokana na wabunge wengi kutoridhishwa na utekelezaji wa
mipango ya wizara yake.
Simbachawene
alikumbwa na hali hiyo jana baada ya kuwasilisha makadirio ya bajeti ya
wizara yake ya Sh bilioni 536.960 kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016, huku
wabunge wengi wakizungumza kwa hisia kutokana na kusuasua kwa miradi ya
umeme.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Richard Ndassa, alisema kamati
yake hairidhishwi na mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa na
kuwataka wabunge kuibana Serikali iweze kutimiza majukumu yake
ipasavyo.
Alisema
wizara hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi, lakini kubwa ni
kutopelekwa kwa wakati fedha za miradi ya umeme vijijini na kuiwezesha
Tanesco licha ya fedha hizo kuidhinishwa na Bunge.
Akichangia
bajeti hiyo, Mbunge wa Singida Magharibi, Mohamed Misanga (CCM),
alishangazwa na hatua ya Serikali kusambaza umeme katika vijiji vya
majimbo yote ya Mkoa wa Singida, isipokuwa jimbo lake pekee na kusema
kuwa huo ni ubaguzi wa wazi.
Hata
hivyo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage, alisimama na
kujibu hoja hiyo akimtaka mbunge huyo kutokuwa na wasiwasi na kusema
anatambua jimbo hilo litapatiwa umeme wa vijiji chini ya mradi wa MCC.
Lakini Misanga alikataa kukubaliana na majibu ya Serikali. “Majibu
haya sijaridhika nayo, huu ni ubabaishaji mwingine, waziri anajua
kabisa Singida tupo katika mpango wa REA, leo anasema tutapata umeme wa
MCC, ni uongo,” alisema Misanga.
Kwa
upande wake, Mbunge wa Kigoma Kusini, Davidi Kafulila (NCCR-Mageuzi),
alisema inashangaza kuona miradi mingi inakwama kutekelezwa kwa kigezo
cha ukosefu wa fedha, huku Serikali ikiendelea kulipa Sh bilioni tano
kwa mmiliki wa Kampuni ya IPTL kila mwezi kinyume cha maazimio ya Bunge.
“Katika
kashfa ya Escrow, tulipitisha maazimio humu ndani, kwamba Serikali
isitishe malipo ya shilingi bilioni tano yanayotolewa kila mwezi kwa
mmiliki wa IPTL.
“Haiwezekani
wabunge tunalia miradi ya umeme imekwama huko vijijini halafu wakati
huo huo singasinga mmoja anachukua bilioni tano azalishe umeme
asizalishe, hizi fedha zingezuiwa zingeenda kutekeleza miradi hii
iliyokwama.
“Mimi
nashangaa wizara imeendelea kukaidi azimio la Bunge, kiti cha spika
kinayumba. Katika moja ya maazimio tulikubaliana Serikali ilete majibu
ya utekelezaji, hadi leo wamekaa kimya na spika anachenga,” alisema Kafulila.
Akijibu
hoja hiyo, Simbachawene alisema katika maazimio ya Bunge hakuna
kipengele kinachosema malipo hayo yazuiliwe na kusema Serikali haiwezi
kufanya hivyo kwa kuwa hilo ni jambo la kisheria.
“Mimi
simjui singasinga anayesemwa hapa, ila ninachojua mimi ni kwamba kuna
mkataba baina ya Tanesco na IPTL, sasa unajiuliza tunaufutaje huu
mkataba, ni vigumu, unaufutaje?
“Sheria
ya kampuni, ‘a company is a person, IPTL is a person’, huyo mwingine
anayetajwa naye ‘is a person’. Huyu ‘person’ anayeitwa IPTL hawezi
akaathiriwa hivi hivi tu, tutashitakiwa kama taifa, tutalipa gharama
kubwa kuliko hizo unazosema.
“Na
mifano mnaifahamu, tumepoteza fedha nyingi kwa kulipa kutokana na
maamuzi mabaya, sasa mimi naomba Bunge lituambie tutekelezeje? Bunge
lituambie sasa nyinyi kutokana na jambo hili liko hivi fanyeni hivi, ili
likitokea jambo huko tusijekuulizwa.
“Mimi
nilikuwa mjumbe wa kamati na Tundu Lissu (Mbunge wa Singida Mashariki),
hilo azimio analosema Kafulila kila siku la kusimamisha haya malipo ya
‘capacity charge’ halipo katika maazimio nane, labda kiti kitusaidie,
kama hilo azimio lipo huko kwenu tupeni,” alisema Simbachawene.
Hata
hivyo Mwenyekiti wa Bunge, Musa Azan Zungu kabla ya kumruhusu Kafulila
kufunga hoja yake, alisema hawezi kuruhusu mjadala huo uendelee kwa kuwa
suala hilo lipo mahakamani.
“Hili
suala lipo mahakamani, najua ‘concern’ (dhamira) ya Kafulila ni ‘very
banning’ (nyeti), lakini kuna masuala ya kisheria na mimi kama refa
nafuata taratibu za kibunge.
“Naelewa
sana hoja yako Kafulila, nimeiacha ili upate ‘comfort’, lakini kiti
hakiwezi kuruhusu mjadala huu uibuke upya wakati mambo haya
tulishafanyia uamuzi, na kwa mujibu wa kanuni zetu jambo likishafanyiwa
uamuzi haliwezi kurudiwa,” alisema Zungu.
0 comments:
Post a Comment