MWENYEKITI
wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu, amesema anayo nia na uwezo
wa kumwangusha Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema) katika
Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba.
Kauli
hiyo aliitoa mjini hapa jana ikiwa ni siku tatu baada ya Makamu
Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Phillip Mangula, kumaliza mgogoro wa
kisiasa uliosababisha baadhi ya wanachama wa chama hicho Iringa Mjini
wafukuzwe uanachama huku Msambatavangu akipewa onyo kali.
Machi
mwaka huu, vikao vya chama hicho ngazi ya wilaya na mkoa viliwafukuza
uanachama Shukuru Luhambati, Clara Shirima na Hosea Kaberege huku
Msambatavangu akipewa onyo kali lililodaiwa kumwondolea sifa ya kugombea
nafasi yoyote ya uongozi kupitia chama hicho na kuzusha hofu ya
mpasuko.
Akizungumzia
rufaa walizokata na uamuzi aliokuja nao Mangula na kuwasilisha katika
kikao cha Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, alisema:
“CCM
kwa kutumia kanuni na katiba yake imepitia rufaa zetu, ikajifunza kitu
na kutumia busara yake kutupilia mbali adhabu hizo ili kulinda masilahi
mapana ya chama hiki.
“Tunajiandaa
kushiriki Uchaguzi Mkuu tukiwa wamoja na niwahakishieni mimi ni mmoja
kati ya wana CCM wenye nia ya kugombea ubunge katika Jimbo la Iringa
Mjini.
“Sijajua makada gani wengine watajitokeza wenye uwezo wa kusema ni nani, ni CCM wenyewe na wananchi wa jimbo hili.
“Kwa
mimi kutangaza nia na kujitoa nina hakika na ninafahamu nina uwezo wa
kupeperusha bendera na kurudi na ushindi, sitailetea aibu CCM na nipo
tayari kumuunga mkono mgombea atakayeteuliwa.”
Alitaja
kipaumbele chake cha kwanza endapo CCM itampa ridhaa ya kuwania nafasi
hiyo kuwa ni elimu na katika sekta hiyo atakahikisha miundombinu yake
inaboreshwa ili iwe ya kisasa.
Alisema
katika kuboresha ustawi wa elimu, atahakikisha vijana wengi wa shule za
msingi na sekondari za Iringa Mjini wananufaika kwa uwapo wa vyuo vikuu
vinne vya mjini hapa kwa kutengeneza ushirikiano utakaosaidia vijana
wengi kujiunga na elimu ya juu.
Msambatavangu
alisema licha ya CCM kuwa wapinzani katika jimbo hilo, lakini bado wana
nguvu ya kutosha kisiasa na ndiyo maana walipata viti vingi katika
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Katika uchaguzi huo, CCM ilipata viti 126, Chadema 64 na CUF kimoja.
Kama
atatimiza azma yake hiyo, Msambatavangu ambaye ni msomi mwenye Shahada
ya Uzamili ya Usimamizi wa Biashara atakuwa anaingia kwa mara ya pili
katika kinyang’anyiro hicho.
Katika
kura za maoni ndani ya CCM zilizoshirikisha wagombea 12 mwaka 2010,
alikuwa mtu wa nne baada ya kupata kura 916 nyuma ya Frederick
Mwakalebela aliyepata 3,897, Monica Mbega 2,989 na Dk. Yahaya Msigwa
1,217.
0 comments:
Post a Comment