Marehemu Chacha Wangwe |
MTOTO
wa marehemu, Chacha Wangwe, Zakayo Wangwe, ambaye alitangaza nia ya
kugombea ubunge Jimbo la Tarime hivi karibuni, amebadili mawazo na
kutangaza kugombea udiwani Kata ya Turwa.
Uamuzi huo aliuchukua jana na kuwaeleza waandishi wa habari kwamba, amejitathmini na kuona agombee udiwani badala ya ubunge.
“Nimepokea
simu na meseji nyingi kutoka kwa watu wangu wa karibu, wengine
wamenishauri lakini mwisho wa siku naweka wazi kwamba nia yangu ya
kugombea ubunge nimeona niachane nayo ila nigombee udiwani.
''Yapo
mambo mengi yaliyotokea baada ya kutangaza nia yangu ambayo kimsingi
nayachukulia kama mapambano ya kisiasa licha ya kuwa na athari hasi
kwangu, lakini maamuzi yangu sasa ni udiwani,'' alisema Zakayo.
Zakayo
alisema uamuzi huo umetokana na ushauri mwingi kutoka kwa familia,
ndugu, marafiki, wanachama wenzake wa Chadema na watu mbalimbali kutoka
ndani na nje ya Tarime wa kumtaka kugombea udiwani badala ya ubunge kama
ilivyokuwa kwa marehemu baba yake, Wangwe.
Alisema
wakati wa uhai wa baba yake, aliwahi kushauriwa kugombea udiwani badala
ya ubunge na kukubali na alifanikiwa kupata na baadaye aligombea ubunge
na kushinda, hivyo anafuata nyayo za baba yake.
“Ningeweza
kusimamia msimamo wangu hasa baada ya majimbo kugawanywa, lakini
natambua fika thamani ya busara, nasaha na maono ya watu wanaonizunguka,
natambua pia kiongozi bora ni yule aliye msikivu na aliye tayari
kukosolewa na wananchi wenzake,” alisema.
0 comments:
Post a Comment