BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Watanzania limewasimamisha wabunge 11 kwa kudharau mamlaka ya Spika jana.
Hatua hiyo ni baada Spika wa Bunge hilo, Anne Makinda, kuwashitaki
katika Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge,
wabunge hao wa Kambi Rasmi ya Upinzani, wakiongozwa na Mnadhimu Mkuu wa
Kambi hiyo, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema).
Makinda alichukua hatua hiyo, baada ya wabunge hao kurudia kwa mara
ya pili kufanya vurugu na kupiga kelele wakati kikao kikiendelea na
kumlazimisha kuahirisha kwa mara ya nyingine shughuli za bunge
zilizokuwa zikiendelea bungeni mjini hapa.
“Bunge haliwezi kuendeshwa kwa kelele na vurugu namna hii. Kwa mujibu
wa Kanuni za Bunge, ninawataja kwa majina vinara wa vurugu ambao
walitakiwa kufika kwenye Kamati ya Maadili na kulazimika kuahirisha
Bunge hilo hadi jioni."
Hukumu ya Watuhumiwa
Kamati hiyo ilitoa adhabu kwa mafungu matatu ambapo wapo ambao
hawakutoa ushirikiano kabisa kwa kamati hiyo wakidai wangefanywa hivyo
mbele ya wanasheria wao, hao walifungiwa moja kwa moja, waliotoa
ushirikiano kwa kamati wakafungiwa kutohudhuria vikao viwili na wengine
waliochelewa kupata wito wanatakiwa kuhojiwa na kama leo asubuhi saa nne
wakati mmoja hakuguswa na adhabu hizo kabisa.
Waliosimamishwa moja kwa moja ni Lissu, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika
(Chadema), Mbunge wa Viti Maalumu, Paulina Gekul (Chadema), Mbunge wa
Mohambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) na Mbunge wa Kasulu Mjini na
Moses Machali (NCCR-Mageuzi).
Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), Rashid Ally Abdallah
(CUF) na Mbunge wa Gando, Khalifa Khalifa (CUF), hao wanatakiwa kufika
katika kamati hiyo ya maadili leo kwa kuwa hawakupata wito wa kuitwa
jana mapema huku Mbunge David Silinde hakuguswa kabisa katika adhabu
hiyo.
Kundi la pili waliofungiwa vikao viwili, cha leo na Jumatatu ni
Mbunge wa Ole, Rajab Mbaruk Mohamed (CUF) na Mbunge wa Iringa Mjini,
Peter Msigwa (Chadema) ambao waliitikia wito na walitoa ushirikiano kwa
Kamati hiyo ambayo Makamu Mwenyekiti wake ni Brigedia Hassan Ngwilizi,
ambaye ni Mbunge wa Mlalo (CCM).
Akiwasilisha maamuzi ya kamati hiyo, Mwenyekiti wa kamati alisema
walifikia maamuzi hayo baada ya kuridhika baada ya kuwaita wahusika na
kujieleza na hatimaye kufikia maamuzi hayo.
Kamati hiyo ambayo Makamu Mwenyekiti wake ni Kapteni John Chiligati,
ambaye ni Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM) ilitoa maamuzi hayo
kulingana kanuni za Bunge.
Ilivyokuwa
Vurugu hizo zilianza mara baada ya Lissu kusimama kuomba Mwongozo wa
Spika, wakati Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alipokuwa
akisoma kwa mara ya pili, muswada wa Sheria ya Mafuta na Gesi wa mwaka
2015, ambao Kambi ya Upinzani ilikuwa ikiupinga tangu mwanzo.
Wakati wakipiga kelele, Spika alinyamaza na Simbachawene akaendelea
kusoma muswada huo, ndipo wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani wote
waliokuwepo bungeni wakasimama kumuunga mkono Lissu na kuwalazimu baadhi
ya wabunge wa CCM kuanza kuwazomea na wao kurudisha maneno
yaliyosababisha hata aliyekuwa akisoma asisikike.
Msimamo wa upinzani
Pamoja na yaliyotokea, kambi hiyo ilijikusanya ndani ya Bunge hilo
kupeana misimamo ambapo, walisikika wakisema hata iweje, hawatakubali
muswada huo wa Sheria ya Mafuta na Gesi upite.
Katika hatua nyingine, Spika Makinda alikataa kuendekeza malalamiko
ya Mbunge wa Viti Maalum, Martha Mlata (CCM), aliyeomba mwongozo na
kudai kuwa, Mbunge wa NCCRMageuzi, Moses Machali alimdhalilisha kwa
kumwambia kuwa, alifumaniwa na wajinga wenzake.
Machali alisema hivyo alipokuwa akitoa maoni ya muswada uliopitishwa
wa Ulinzi wa Mtoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi, baada ya kukasirishwa
na kitendo cha Mlata kuropoka kuwa Mbunge huyo aliyetaka adhabu iwe
kunyongwa ni kichaa.
“Leo wote mmeonesha utovu wa nidhamu wa hali ya juu, kwa kutoleana
maneno yasiyofaa. Wengine mmekuwa mkiingilia hoja za wenzenu wakati
wanaziwasilisha, kwa kuwatolea maneno yasiyo na adabu,” alisema.
0 comments:
Post a Comment