Pages

Ads 468x60px

Sunday, June 11, 2017

Mauaji Kibiti: IGP Sirro Awataka Waandishi Kuwa Wazalendo

Wakati  Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba akisema matukio ya mauaji ya hivi karibuni mkoani Rufiji yana harufu ya kisiasa, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro amevitaka vyombo vya habari kuwa na uzalendo, ikiwa ni pamoja na kuacha kutoa taarifa zenye kuchochea hofu kwa wananchi.

Waliyasema hayo kwa nyakati tofauti juzi na jana katika mikoa ya Singida na Morogoro. Waziri Mwigulu Akihutubia wananchi katika Kijiji cha Kaselya wilayani Iramba, Singida juzi katika siku ya kwanza ya ziara ya siku tatu kutembelea jimbo lake, Mwigulu alisema anahusisha mauaji hayo na siasa kwa kuwa mauaji ya wananchi kwenye maeneo hayo yanawakumba zaidi wafuasi na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alihoji; “Ujambazi gani huo wa Wana CCM tu? Hako kamchezo tumeshakagundua. Dhahiri, huo ni ushamba wa vyama vingi.” Alisema wanaodhani kuwa upinzani ni kwenye maisha wanakosea. “Naomba tupingane kwa kushindanisha sera na wala tusikunjiane ngumi kwa ajili ya siasa kwa kuwa siasa haipaswi kuwa ya uadui,” alisema.

Alisema pamoja na siasa hazipaswi kuwa ya uadui bado wapo baadhi ya wapinzani wanaotengeneza siasa ili zionekane kuwa ni za uadui. “Watu hawa wangekuwepo wakati wa vita baina ya nchi yetu na Uganda, hakika wangemsaidia Iddi Amin; bahati nzuri walikuwa bado wadogo,” alisema Waziri.

Sirro na uzalendo 
Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) nchini, Sirro amevitaka vyombo vya habari nchini kuwa na uzalendo ikiwa ni pamoja na kuacha kutoa taarifa zenye kuchochea hofu kwa wananchi.

Alitoa rai hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro ambapo alisema baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikitumia maneno yanayoongeza hofu kwa wananchi.
Kuhusu mauaji yanayotokea katika wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga mkoani Pwani, alisema vyombo vya dola vinaendelea kuyadhibiti na kwamba, jeshi hilo linaendelea kuchukua hatua, lakini baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikitoa taarifa za kuchochea hofu.

“Taarifa zinazotolewa kwa umma hazioneshi kama kuna kazi inafanyika na vyombo vya dola kuzima mauaji hayo,” alisema 
Aidha, alisema pamoja na habari hizo kujenga hofu kwa jamii, pia zimekuwa zikiambatana na picha za watu waliojeruhiwa, picha za silaha kuonesha Pwani ni eneo la vita.

IGP Sirro aliwataka wanahabari wanapoandika masuala ya kiusalama, watafute ufafanuzi kwenye vyombo husika ili waandike taarifa sahihi, ikiwa ni pamoja na kutanguliza uzalendo mbele huku wakitambua athari zinazotokana na taarifa hizo kwa jamii.

Alisema wananchi wakijawa na hofu, watashindwa kutekeleza shughuli zao za kijamii na kiuchumi. “Epukeni sana kuandika habari zenye sura ya kishabiki kwenye suala hili, habari nyingi mnazoandika kwenye suala hili mnaonesha kama vile mnalifurahia, hili si suala la kufurahia hata kidogo,” alisema 
Alisema hayo ni mapambano hivyo kila mmoja anawajibika katika kusaidia ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kuzuia uhalifu na kuwakamata wahalifu.

0 comments:

Post a Comment

SHARE