Waziri
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema salfa
iliyoingizwa nchini kwenye makontena 211 haina kasoro na inafaa kwa
matumizi ya kupulizia kwenye mikorosho.
Majaliwa
amesema hayo wakati akizungumza na wajumbe wa kamati maalum, waagizaji
wa salfa na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Korosho nchini (CBT) kwenye
kikao alichokiitisha kwenye makazi yake, Oysterbay, jijini Dar es
Salaam.
“Bodi
kaandaeni taratibu za kawaida kusambaza salfa kwa wakulima ili waanze
kupuliza dawa hiyo. Wasichelewe kupuliza kwa sababu msimu umeshaanza,” amesema.
Juni
4, mwaka huu Waziri Mkuu alimuagiza Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof.
Samuel Manyele aende kuchunguza mzigo wa salfa ulioko bandari ya Dar es
Salaam baada ya kutokea mkanganyiko uliosababishwa na ripoti ya TPRI
kuwa ya salfa iliyoingizwa nchini na kampuni ya ETG Inputs Ltd kwa niaba
ya Bodi ya Korosho haijakidhi viwango.
Waziri
Mkuu alichukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa kuna mkanganyiko
miongoni mwa wakulima juu ya matumizi ya kiuatilifu hicho licha ya kuwa
Serikali ilikwishapokea taarifa ya bodi, na taarifa ya kampuni
iliyotengeneza salfa hiyo na taarifa iliyoletwa na mwagizaji ambayo
imethibitishwa na makampuni matatu ya kimataifa. Aliyataja makampuni
hayo matatu kuwa ni InterTech, Bureau Veritas na SGS.
Akitoa
taarifa ya uchunguzi wao mbele ya Waziri Mkuu, Prof. Manyele alisema
walifanya uchunguzi kwenye makontena 21 ambayo ni sawa na asilimia 10 ya
makontena yote 211 ili kubaini ubora wake.
“Uchunguzi
ulifanyika kwenye maeneo ya purity, acidity na moisture contents kama
ulivyokuwa umeelekeza. Sampuli zilichukuliwa kutoka GALCO Inland
Container Depot iliyoko Chang’ombe ambako ndiko mzigo wa salfa ulioletwa
na kampuni ya ya ETG Inputs Ltd unahifadhiwa,” alisema.
“Kwa
kuzingatia matokeo ya kiuchunguzi wa kimaabara uliofanyika, viwango
(specifications) vilivyowekwa ndani ya mkataba na viwango vya Shirika la
Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kuhusiana na kiuatilifu cha salfa ni
maoni yetu kuwa mzigo wa salfa ulioko ndani ya makasha (containers) 211
unakidhi viwango,” alisema kwenye taarifa yake.
Naye,
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho nchini, Bw. Maokola Majogo alisema
yeye pamoja na Bodi yake watatekeleza maelekezo ya Waziri Mkuu na
akawataka wakulima wasisite kutumia salfa hiyo kwani
imekwishathibitishwa na Mkemia Mkuu kwamba haina matatizo.
0 comments:
Post a Comment