KWA UFUPI
Pemba/Dar.
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ameitaka CCM kujiandaa
kisaikolojia kukabidhi madaraka kwa chama chake baada ya Oktoba, akisema
katika chama chake hakutakuwa na neno “kushindwa”.
Maalim Seif, ambaye
pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, aliwataka vijana popote
walipo kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi ili kujitayarisha na ushindi
aliouita mkubwa.
Alitoa kauli hiyo
katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Tibirinzi,
Chake Chake Pemba na kuhudhuriwa na maelfu ya wafuasi wa chama hicho
kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar.
“Hakuna kushindwa
CUF, kwa hivyo mawazo yenu yawe na kushinda tu. Vijana, hakuna kukaa
ukasema ushamaliza kupiga kura, unakwenda kwako unasubiri ushindi.
Hakuna hilo mwaka huu, lazima mjitahidi kulinda ushindi wenu,” alisema
Maalim Seif.
Katibu huyo wa CUF
alisema wananchi wa Pemba walioko Arusha, Mwanza na sehemu nyingine
warudi kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura na kuwataka kutoacha
fursa hiyo ambayo ni haki yao ya kidemokrasia.
Akitilia mkazo
suala hilo, aliyekuwa waziri wa SMZ, Mansoor Yussuf Himid alimtaka
Maalim Seif baada ya kupiga kura yake kurudi nyumbani na kuwaachia
vijana kumkabidhi ushindi wa chama hicho.
Mansoor ambaye ni
mshauri wa Maalim Seif, alisema vijana wasitarajie kuletewa ushindi
katika kisahani cha chai, washiriki kikamilifu katika kupatikana ushindi
wa chama hicho.
Mansoor alisema
hatima ya ushindi wa Zanzibar ipo mikononi mwa vijana, hivyo wanapaswa
kuhakikisha ushindi wa Zanzibar unapatikana katika ya mikono yao.
Akihutubia mkutano
huo, Mwanasiasa Hassan Nassor Moyo alisema kazi ya Maalim Seif na
aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume kuleta umoja wa kitaifa
si jambo jipya kwa kuwa lilianzia kwa Mzee Karume ambaye alitunga sheria
kuondosha ubaguzi na kuwaweka wananchi wote wa Zanzibar kuwa kitu
kimoja.
Uchumi
Katika hotuba yake
ya takriban saa moja iliyorushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni
cha Star TV, Maalim Seif alisema Maalim Seif alisisitiza nia yake ya
kuifanya Zanzibar kuwa na mamlaka kamili ili iondokane na adhabu ambazo
siyo stahiki kwake.
Seif alisema Wazanzibari wamekuwa wakiadhibiwa kutokana na ufisadi unaofanywa na baadhi ya viongozi wa Bara.
“…Leo watu
wanafanya ufisadi huko, tunanyimwa fedha na wahisani halafu sisi ndiyo
tunaadhibiwa kwa makosa ambayo siyo ya kwetu. Hatuwezi kukubali,”
alisema Seif na kusisitiza kuwa hali hiyo imesababisha bidhaa kupanda
bei na kuwaumiza zaidi Wazanzibari.
“Zanzibar haina
mamlaka kwenye nchi nyingine, hatuwezi kufungua ubalozi kwenye nchi
nyingine. Hatuwezi kusaini mkataba na nchi yoyote, hatuna maamuzi juu ya
sera, hatuna sera za kiuchumi. Sera zote zinatungwa Dar es Salaam… hii
siyo sawa,” alisema Seif.
“Leo tukizungumzia
suala la gawio tunapata asilimia 4.5 badala ya asilimia 11.5…ndiyo maana
nasema Muungano uliopo hautusaidii. Tutapata kufaidika pale
tutakapotapa mamlaka kamili. Zanzibar iwe na mamlaka yake na Tanganyika
iwe na mamlaka yake. Halafu tukae pamoja tuangalie pale tunapoweza
kushirikiana tushirikiane.
“Kwani Tanganyika
haiwezi kwenda bila Zanzibar… kwani kuna nini hapa,” alihoji Seif huku
akishangiliwa na umati wa watu waliohudhuria mkutano huo.
“Eti wanaokuja
Zanzibar kutafuta wadhamini wanasema watawadhibiti wanaovuruga Muungano.
Watawadhibiti hao CCM wenzao siyo sisi… tunataka uhuru wetu. Tunataka
tupate mamlaka kamili.”
Maalim Seif, ambaye
alitamba kuwa ameteuliwa kwa mara ya tano kuwania urais kuwa kuwa
anaaminika, alisema mpango wake ni kuboresha Bandari ya Zanzibar ndani
ya mwaka mmoja na kuitangaza kuwa huru.
Alisema atahakikisha Zanzibar inakuwa na viwanja viwili vya kimataifa vya ndege.
Alisema ushindi wa
chama hicho utakuja na mabadiliko ya kiuchumi yatakayowezesha
kuimarishwa bandari huru katika kisiwa cha Pemba katika maeneo ya Mkoani
na Wete akifafanua kuwa Pemba imekosa maendeleo tangu wakati wa ukoloni
hivyo kuna haja ya kuimarishwa kiuchumi na kuendelezwa ili vijana
waweze kufaidika na matunda ya nchi yao kwa kupatiwa ajira.
“Lazima tuwe na
meli za kisasa za kasi ili kuimarisha usafiri na miundombinu kuwawezesha
wananchi kuvusha biashara zao, alisema Maalim Seif ambaye safari hii
anawania urais wa Zanzibar mara ya tano.
Katika mkutano huo wanachama 400 walichukua kadi za chama hicho baada ya kuhama kutoka ADC.
Imeandikwa na Mwinyi Sadallah, Salma Said (Pemba) na Susan Mwillo (Dar)
0 comments:
Post a Comment