MWANAMUME mmoja ameuawa na mwili wake kuchomwa moto na wananchi wenye
hasira katika wilaya ya Bunda mkoani Mara, kwa tuhuma ya kuiba kuku
mmoja.
Kwa mujibu wa polisi wilayani Bunda, tukio hilo limetokea juzi majira ya
asubuhi mjini Bunda. Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama katika
wilaya ya Bunda, ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, Lydia Bupilipili,
jana amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Alisema mwanamume huyo aliuawa na wananchi wanaojiita wenye hasira,
baada ya kumkamata akiwa ameiba kuku mmoja, mali ya mkazi wa mjini hapa.
Amemtaja aliyeuawa kwa kipigo na wananchi hao na kisha mwili wake
kuchomwa moto kuwa ni Mwita Machanchu (30) mkazi wa Mtaa wa Mapinduzi
mjini Bunda.
Hata hivyo, akizungumza baada ya kuzindua Bodi ya afya ya halmashauri ya
wilaya ya Bunda, mkuu huyo wa wilaya alikemea vitendo vya mauaji
vinavyotokea mara kwa mara wilayani Bunda.
Alisema kitendo cha watu kujichukulia sheria mkononi na kuondoa uhai wa
watu wengine, kamwe hakivumiliki na akawataka wananchi pindi
wanapowakamata wahalifu wawafikishe polisi, ili wafikishwe hatua za
kisheria zichukue mkondo wake.
Aidha, amewataka wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa jeshi la
polisi na kwenye kamati ya ulinzi na usalama, kwa kuwataja watu
wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu ili waweze kukamatwa na kufikishwa
mahakamani.
0 comments:
Post a Comment