Pages

Ads 468x60px

Saturday, May 30, 2015

Viongozi Afrika Mashariki kuijadili Burundi Dar



VIONGOZI wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanatarajia kukutana kesho Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili msimamo wa Burundi wa kuendelea na uchaguzi wakati bado nchi hiyo ipo kwenye machafuko.
 
Taarifa hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Dk.Mary Mwanjelwa (CCM).
 
Katika swali lake Dk. Mwajelwa alitaka kujua msimamo wa Tanzaniua  kuhusu uamuzi wa Burundi kuendelea na uchaguzi Juni 26, mwaka huu, licha ya kuwepo kwa machafuko.
 
Mbunge huyo alisema machafuko hayo yamesababisha wakimbizi zaidi ya 51,000 kuingia nchini na kuisababisha nchi hasara.
 
Membe alisema ni kweli  baada ya machafuko kutokea Mei 6 mwaka huu na jaribio la kutaka kumuondoa madarakani Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, Rwanda ilipokea wakimbizi wasiopungua 150,000 na Tanzania ilipokea wakimbizi 51,000.

“Wakimbizi hawa waliingia kwenye maeneo yetu na kusababisha uharibifu mkubwa hasa kwenye shule za msingi, mazao na mifugo.

“Hali hii imesababisha Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk. Jakaya Kikwete kushughulikia utatuzi wa suala hili.

“Kuhusu suala la uchaguzi wa Juni 26 mwaka huu Viongozi wa Afrika Mashariki wanakutana keshokutwa (kesho) Dar es Salaam ili kulishughulikia tatizo la usalama na hali ya uchaguzi nchini Burundi,” alisema.

Membe alisema msimamo wa Tanzania ni kwamba wanaitaka  Burundi na hasa Warundi watulie wayamalize matatizo yao ndani.

“Jumuiya ya Afrika Mashariki itakuwa tayari kuwasaidia kuondokana na tatizo hili ambalo linatuletea wakimbizi nchini.

“Tanzania tunaamini amani ya Burundi ni amani ya Tanzania kwa hiyo tutawasaidia kwa lolote lile ili kuhakikisha amani ya Burundi inarejea,” alisema Membe.

0 comments:

Post a Comment

SHARE