Pages

Ads 468x60px

Sunday, June 28, 2015

ACT-Wazalendo Kurudisha Mashamba ya Mkonge kwa Wananchi



CHAMA cha ACT-Wazalendo kimesema kina shabaha ya kurejesha kwa wananchi mashamba ya mkonge yaliyouzwa kwa matajiri wachache ambao kwa sasa hawayatumii kwa kilimo cha zao hilo.
 
Pia chama hicho kimeazimia kurejesha Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) wa Watanzania ili nchi iweze kujitegemea kiuchumi.
 
Kauli hiyo imetolewa juzi na Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe akiwa jijini Tanga alipokuwa akikitambulisha chama hicho kipya kwa wananchi.
 
“Mwaka 2014 mkonge umechangia dola za Marekani milioni 16 katika mauzo ya bidhaa nje, hiki ni kiwango kidogo mno, mashamba yapo lakini yameuzwa kwa matajiri wachache na hayazalishi.
 
“Chama chetu kinataka mashamba haya waliyouziwa matajiri ambayo hayazalishi wapewe wananchi, Azimio la Tabora limetamka hilo kinaga ubaga,” alisema Zitto.
 
Alisema ardhi na mashamba yote yaliyokuwa ya mashirika ya umma na kubinafsishwa yarejeshwe kwa wananchi wasio na ardhi kwa kuwagawia na kushiriki katika uzalishaji kwa kutumia mfumo wa ‘out growers scheme’.
 
Zitto alisema mashamba makubwa ya kibiashara yatakapohitajika itakuwa ni jumla ya mashamba madogo madogo ya wananchi na pale uwekezaji utakapohitaji basi wananchi watamiliki theluthi mbili ya shamba husika na mwekezaji wa ndani au wa nje atamiliki theluthi moja tu.
 
“Tunataka mkonge ulimwe na wakulima wadogo ili Watanzania wawe na shughuli za kilimo zenye tija,” alisema.

Akizungumzia mabenki, alisema Azimio la Tabora limeagiza dola kumiliki benki kubwa nchini ili kujitegemea kiuchumi kwani nchi haiwezi kuendelea iwapo mabenki makubwa yote yanamilikiwa na watu kutoka nje.
 
Zitto alisema malengo ya kujenga uchumi shirikishi wenye uhuru mkubwa katika soko la mitaji hayawezi kufikiwa bila ya kuwa na benki zinazomilikiwa na Watanzania wenyewe.
 
Alisema ACT-Wazalendo itahimiza Benki ya Taifa ya Biashara irejeshwe kwenye mikono ya Watanzania kwa kumilikiwa na Serikali kwa asilimia 50 na wananchi na taasisi za wananchi kupitia soko la mitaji nusu iliyobakia.
 
Zitto alisema chama chao kitahimiza pia Benki ya Maendeleo na Benki ya Kilimo kuwa na muundo wa umiliki kama wa NBC.
 
Kiongozi huyo alisema ubinafsishaji wa NBC ulifanywa holela na benki iliuzwa kwa bei ya bure, na kwamba msimamo huo wa chama chao unaungwa mkono na kazi iliyofanywa na Kamati ya Bunge ya PAC iliyoagiza ukaguzi maalumu kwenye mchakato wa ubinafsishaji huo. 
 
“Tunataka kurejesha nafasi ya Tanga kwenye taifa letu. Tunaomba muunge mkono chama chetu, tunawakabidhi chama hiki watu wa Tanga, ni chama chenu na kiwe jukwaa lenu katika kupaza sauti za wanyonge. 
 
“Tanga ni mkoa uliokuwa mstari wa mbele katika kulikomboa taifa letu. Chama cha TANU kilisheheni viongozi kutoka Tanga. Kina Stephen Muhando na Mwalimu Kihere kwa nyakati tofauti walikuwa watendaji wakuu wa TANU wakati tunasaka uhuru wa nchi yetu,” alisema.
 
 Zitto alisema Tanga bado ina nafasi kwenye uchumi wa nchi, inashika nafasi ya 8 katika mchango kwa pato la taifa, unashika nafasi ya 3 katika makusanyo ya kodi nchini baada ya Dar es Salaam na Arusha.

0 comments:

Post a Comment

SHARE