WAKATI makada watano wakiwa wamejitokeza kutangaza nia ya kuwania urais kwa tiketi ya chama tawala, CCM, leo ni zamu ya Waziri wa Nishati na Madini aliyejiuzulu, Profesa Sospter Muhongo.
Kwa mujibu wa kambi ya mwanajiolojia huyo maarufu duniani, atatangaza
dhamira yake hiyo akiwa katika ukumbi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania
(OUT) Tawi la Musoma mkoani Mara.
Muhongo aliyejipatia umaarufu mkubwa wa uchapaji kazi akiwa waziri,
anatajwa kujielekeza zaidi katika kuiweka Tanzania kuwa nchi ya uchumi
wa kati, hasa kwa kutumia rasilimali ya nishati ya gesi iliyogunduliwa
nchini.
Kiongozi huyo ambaye kwa sasa amebaki na kofia yake ya mbunge wa
kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, aliachia ngazi hivi karibuni kutokana
na sakata la Escrow.
Hata hivyo, tume zilizoundwa kuchunguza sakata hilo, zilimsafisha yeye na Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi.
Muhongo anatarajiwa kuungana na Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa, Waziri wa Kilimo, Chakula la Ushirika, Stephen Wassira, Naibu
Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi
Maalumu) Profesa Mark Mwandosya na Mbunge wa Afrika Mashariki, Charles
Makongoro Nyerere waliotangaza nia.
Kesho itakuwa zamu ya Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, ambaye
kwa sasa ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja. Ngeleja anatarajiwa
kutangaza nia jijini Mwanza.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani anatarajiwa kutangaza nia
wakati wowote wiki hii. Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe anatarajiwa kutangaza nia kijijini kwake Rondo
mkoani Lindi Jumamosi wiki hii.
Akizungumza wakati wa Tamasha la Kaswida jijini Dar es Salaam
mwishoni mwa wiki, Membe aliyekuwa mgeni rasmi siku hiyo alithibitisha
kutaka kutangaza nia hiyo na kuwaomba wananchi wamsikilize kwa makini
siku hiyo, kwa kuwa ataeleza kwa kina nini anataka kufanya nchi iweze
kuondoka ilipo na kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo.
0 comments:
Post a Comment