Mio za kuwania kumrithi Rais Jakaya Kikwete miongoni mwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimezidi kushika kasi, safari hii Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, akinusurika kifo baada ya ndege aliyokuwa akisafiria kuwapo katika hatari ya kugongwa na ndege nyingine angani alipokuwa akielekea Zanzibar.
Waziri Membe akiwa na ujumbe wake wa watu nane walikuwa wakisafiria
ndege ya kukodi kampuni ya 5H NEG Precision Aviation ikirushwa na rubani
Mathew Mhahiki ambaye ameonesha kushangazwa na tukio hilo alilodai “ni
kwa rehema za Mungu tumepona ajali hii.”
Akizungumza na mwandishi wetu, rubani Mathew Mhahiki alisema, “…lazima
kuna tatizo katika control center hata hivyo tayari nimeongea nao na
wameniomba samahani na kudai walipitiwa maana kwa hali ilivyokuwa ni
kwamba tungegongana wakati wa kutua, nimeshangaa tu kuona ndege hii hapa
ndio maana nikaamua kumkwepa mwenzangu nikapanda juu.”
Aidha, Waziri Membe aliyeonekana kushitushwa na hali hiyo alisema,
“…nina uzoefu mkubwa wa kusafiri na ndege mahali pengi duniani, hali hii
ilikuwa ni ajali na labda sasa tungekuwa dead bodies lakini ninajua
Mungu yuko upande wetu katika safari hii ya uhakika, lakini pia
izingatiwe nimekuja kufanya kazi ya Mungu.”
“Katika safari hii tutashuhudia mambo mengi sana lakini kwa kuwa kila
ninapotaka kuondoka nyumbani ama hotelini mara nyingi nimekuwa
nikimtanguliza Mungu maana bila Mungu, hii ilikuwa ni mwisho wa maisha
yetu tuliokuwa kwenye ndege hii,” alisema Membe
Naye mwanasiasa anayenyemelea Ubunge Jimbo la Rungwe Mashariki, Richard
Kasesela, aliyeongozana na Waziri Membe alionesha wasiwasi wa hali hiyo
kuwa inaweza kuwa ni hujuma dhidi ya Membe.
“Katika hali ya kawaida watu wa control center hawawezi kuruhusu ndege
mbili kutua kwa wakati mmoja maana tafsiri yake ni kuwa mtagongana na
ndio maana kuna haja ya kujua ni kwa nini hali hii imetokea katika
kipindi hiki cha Waziri Membe na wanasiasa wengine wanapotafuta kuungwa
mkono kugombea nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi,” alisema
Kasesela
Taarifa nyingine kuhusu tukio hilo zinabainisha kuwapo kwa uzembe
katika chumba cha kuongozea ndege ambapo mmoja wa wafanyakazi katika
chumba hicho alithibitisha uzembe huo.
“Mimi si msemaji wa ofisi yetu lakini hata sisi tumeshangazwa na hali
hiyo maana si jambo la kawaida kutokea kama hakuna tatizo. Wengine
tayari tulishika vichwa maana uzoefu unaonesha kuwa ukiruhusu ndege mbili
kutua kwa wakati mmoja ni wazi unataka kusababisha ajali,” alisema kwa
sharti la hifadhi ya jina.
Waziri Membe alikuwa amealikwa mjini Zanzibar na Umoja wa Kinamama wa
Kikristu (UMAKI) wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Zanzibar, waliokuwa
wakifanya mkutano wao mkuu unaofanyika kila baada ya miaka mitano
akitokea Iringa ambako alikwenda kutafuta wadhamini ili kumwezesha
kugombea urais kupitia CCM.
Akiwa uwanjani hapa Waziri Membe alikutana na Naibu Waziri wa Fedha,
Mwigulu Nchemba aliyekuja Zanzibar kutafuta wadhamini ambapo makada hao
walipata nafasi ya kuzungumza na kujadiliana masuala ya siasa ndani ya
chama chao.
Akiwa katika mkutano wa kinamama hao, Membe alisema; “Miongoni mwa
mambo yanayonikera ndani ya nafsi yangu ni kuona mwanamke bado anaachwa
nyuma, hili halipendezi ni lazima tuhakikishe wanawake wanapata elimu ya
ufundi stadi maana mwanamke akiwezeshwa hasa katika eneo hili la ujuzi,
wanaweza hata kushinda wanaume wengi.”
“Ni lazima kina mama wawezeshwe kujiajiri ili msiwategemee kina baba
kwa kila jambo lakini pia ili kufikia malengo hayo ni lazima tuwape
elimu kina mama.”
Kina mama hao pamoja na mambo mengine wameonesha miradi mbalimbali
wanayoifanya ikiwa ni pamoja na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali kama
mishumaa, asali iliyosindikwa, vitenge, siagi na bidhaa mbalimbali za
nyumbani.
Membe ameahidi kuwasaidia kumpata mfadhili wa kujenga kituo cha umoja
huo na hasa jengo la utawala huku akisisitiza umoja huo pamoja na mambo
mengine, kujenga kituo cha watoto yatima pamoja na mradi wa maji.
Awali, akiwa mkoani Iringa Membe alisema; “Hebu wapimeni hao wanaokuja
kwenu kwa fedha kutaka kuwanunua ili kuwaunga mkono, ni hatari maana
kama kiongozi utajisikiaje kumtumikia mtu ambaye tayari ulimnunua kwa
fedha”
Aliwataka wananchi kupokea fedha wanazopewa na baadhi ya wanasiasa wanaowania urais lakini akisisitiza wawe na msimamo.
“Hizo ni fedha zenu zichukueni mle lakini muwe na msimamo wa
kutomchagua mtu wa namna hiyo maana hatoweza kuwatumikia maana atakuwa
na haya,” alisema Membe
Akizungumzia vipaumbele vyake endapo atachaguliwa kuwa mgombea urais na
hatimaye Rais wa Tano wa Tanzania, Waziri Membe alisema atahakikisha
nchi inapiga hatua za maendeleo kwa haraka kupitia uchumi wa viwanda
vinavyotegemea kilimo.
“Badala ya kuuza pamba sasa tuuze nguo, badala ya kuuza ngozi sasa
tuuze viatu na kadhalika, uchumi wa namna hii unaweza kutoa ajira kubwa
sana na hasa baada ya kugundulika kwa gesi asilia itakayotusaidia
kuondokana na tatizo la nishati ya umeme,” alisema
0 comments:
Post a Comment