Pages

Ads 468x60px

Friday, July 17, 2015

Magufuli Kuhutubia Mwanza Kesho Kutwa>>



Mgombea  urais kupitia CCM,  Dk. John Magufuli,  anatarajiwa kuwahutubia wakazi wa Mkoa wa Mwanza  keshokutwa  ikiwa ni sehemu ya kujitambulisha.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jana, Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Miraji Mtaturu, alisema  Dk. Magufuli atawasili  Mwanza siku hiyo  mchana  na kwenda moja kwa moja kwenye Uwanja wa Furahisha.

Alisema  Dk. Magufuli atapokewa  na viongozi mbalimbali wakiwamo wa dini, siasa na Serikali na aliwataka wananchi kujitokeza kumsikiliza mgombea wao.

“Ni zamu ya Mkoa wa Mwanza baada ya mgombea huyo kutambulishwa  mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam na Zanzibar.  Baada ya kutoka Mwanza atakwenda mkoani kwake Geita."

Alisema   kutokana na umaarufu wa Dk. Magufuli ambaye aliwahi   kufanya kazi  Mwanza, aliwaomba wananchi wote kufika  wakiwamo  mama lishe, waendesha pikipiki, wanafunzi wa sekondari na vyuo vikuu  vilivyopo jijini .

Mtaturu alizungumzia kauli ya hivi majuzi ya mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale-Mwiru na kusema:

“Nimeshangazwa na kauli iliyotolewa na Kada wa chama chetu,  Kingunge Ngombale Mwiru ya kushambulia Baraza la Wazee wastaafu ambao ni viongozi wetu wa chama na Serikali, akiwatuhumu kuendesha vikao vya mchakato wa kumpata mgombea urais kwa mizengwe na ajenda zao za siri.

“Mzee huyu  aliaminika na kusifika akiwa mwalimu mzuri wa siasa aliyefundisha somo hilo Chuo cha Kivukoni akisisitiza    chama kwanza mtu badaye, sasa tunashangaa leo anageuka na kufikiria  kwa tumbo badala ya akili.”

“Anajivunjia heshima yake  inawezekana amesahau ibara ya 29 ya katiba ya CCM inayotambua wazee.  Hatukutarajia mzee atasema  maneno hayo baada ya mgombea urais wa chama kupatikana…basi angesema awali kwa kushauri,” alisema.

Maturu aliwataka waliokuwa wagombea urais  kuvunja makundi yao na kumuunga mkono mgombea wa chama hicho kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa  Oktoba.

0 comments:

Post a Comment

SHARE