Mlipuko
wa furaha kutoka kwa wabunge uliojitokeza jana wakati Serikali
ilipotangaza kufutwa kwa ada ya mwaka ya leseni ya magari (motor vehicle
licence), ulitosha kuonyesha ukubwa wa kero hiyo uliokuwapo kwa jamii.
Si
kero hiyo tu, kelele za furaha kutoka kwa watunga sheria hao pia
zilisikika kwa wingi ilipotangazwa kufutwa kwa ushuru wa usafirishaji wa
mazao chini ya tani moja, ushuru wa huduma kwenye nyumba za kulala
wageni na kutoza ushuru wa forodha wa asilimia sifuri badala ya 25
kwenye malighafi na vifaa vinavyoagizwa mahsusi kwa matumizi ya
walemavu.
Zaidi
ya mara mbili, Spika wa Bunge, Job Ndugai alilazimika kumtaka Waziri wa
Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kurudia alichokisema au kumwambia
inatosha na anaweza akaishia hapo kwani wabunge wamemuelewa na hana haja
ya kuendelea kuisoma bajeti hiyo.
Ijumaa
ya Juni 2, mjadala mkubwa wa kuondolewa kwa ada ya road license
uliibuka bungeni, kilio cha wabunge kikiwa ni kuwapo kwa magari ambayo
yameegeshwa siku nyingi kutokana na ama ajali au uchakavu wa kutotumika
tena hivyo kuitaka Serikali kuifuta ili kuwapa wananchi nafuu na
kutoendelea kudaiwa.
Hoja
hiyo iliyotolewa na Mbunge wa Busega (CCM), Dk Raphael Chegeni kwenye
kipindi cha maswali na majibu ilichangiwa na wabunge wengi akiwamo Spika
bila kujali itikadi zao za vyama vyao.
Hapakuwa
na majibu ya uhakika siku hiyo kutoka kwa Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango, Dk Ashatu Kijaji ambaye aliishia kusema amelipokea pendekezo
hilo na kwamba baada ya kukamilisha taratibu, Serikali itaona hatua
sahihi za kuchukua.
Wiki
hiyo ikielekea ukingoni, Dk Mpango ametangaza kuifuta sambamba na
malimbikizo yake kwa wote waliokuwa wanadaiwa hivyo kuibua nderemo
miongoni mwa wabunge hao walioonyesha kufurahishwa baada ya kusikilizwa
na kufanyiwa kazi kwa maoni yao. “Serikali inatoa msamaha wa kodi, riba
na adhabu zinazoambatana na madeni yote ya ada hiyo yaliyolimbikizwa kwa
miaka ya nyuma,” alisema Waziri Mpango.
Bunge
lilitawaliwa na kelele za CCM… CCM… CCM mara baada ya waziri huyo pia
kutangaza kufuta ushuru kwenye usafirishaji wa mazao yasiyozidi tani
moja pamoja na kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye vifaa
vya walemavu vinavyotengenezwa nchini.
Ilikuwa
hivyo pia alipotangaza mpango wa kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwa
kutoza asilimia sifuri ya ushuru wa forodha kwenye Mashine za
Kielektroni (EFD) kutoka asilimia 10 zilizokuwapo.
Hali ilikuwa hivyo pia ilipotangazwa kuondolewa kwa tozo kwa nyumba za kulala wageni.
0 comments:
Post a Comment