Pages

Ads 468x60px

Wednesday, June 7, 2017

Msajili wa Vyama Azungumzia Sakata la Maalim Seif Kufungua Ofisi Mpya za CUF

Kutokana na Chama cha Wananchi (CUF) kufungua ofisi mpya za chama hicho katika eneo la Mtaa wa Idrisa Kata ya Mzimuni, Magomeni wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Msajili wa Vyama vya Siasa amesema anaamini chama hicho kinafanya mambo yake kwa kuzingatia sheria.

Jana  Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alisema hajapata taarifa yoyote ya chama hicho, kufungua ofisi mpya zaidi ya kuona katika vyombo vya habari.

“Ukiondoa taarifa za kwenye media sijapata taarifa yoyote kutoka CUF labda wawe wameleta leo (jana), lakini naamini chochote wanachofanya wanaelewa taratibu wataleta taarifa, “ alisema Jaji Mutungi.

Jaji Mutungi alisema sheria inawataka wanapofungua ofisi watoe taarifa ndani ya siku 14, ambazo hazijaisha hivyo anaamini wanajua hilo. 
Upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad wamefungua ofisi hizo, baada ya tukio la kuvamiwa katika Ofisi Kuu za Buguruni na kundi la Profesa Ibrahim Lipumba.

Jaji Mutungi alisema atakapopokea taarifa rasmi ataangalia kama taratibu zilifuatwa kwani ufunguaji wa ofisi mpya una taratibu zake. 
“Nikiletewa taarifa ndio nitajua kama walifata taratibu au la, ufunguaji wa ofisi una taratibu zake najua wanazijua pia, “ alisema Jaji Mutungi.

Alisema taarifa hiyo ataipata kutoka kwa mwenyekiti au msemaji wa chama, ambaye ni katibu mkuu ambao wanatambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa. 
Akizindua ofisi hiyo Juni 4 mwaka huu, Maalim Seif alisema ofisi hiyo imetolewa na wabunge 40 wa CUF.

Alisema uamuzi wa wabunge hao kumpatia ofisi ya kufanyia kazi hapo ni kitendo cha kiungwana na kiungwe mkono na wanachama wote. 
Alisema kwa miezi 10 sasa, wamekuwa wakishindwa kufanya kazi kwa upande wa Tanzania Bara, jambo ambalo limewaathiri hivyo kupatiwa ofisi kutamsaidia kutimiza majukumu bila hofu yoyote.

Katibu huyo alisema ana imani na mahakama kuwa itawapatia haki stahiki hivyo kuwataka wanachama kuendelea kuwa na subira.

0 comments:

Post a Comment

SHARE