Pages

Ads 468x60px

Tuesday, June 13, 2017

Rais Magufuli Akutana na Wakuu Wote wa Mikoa Nchini na Kutoa Maagizi Mazito

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewaagiza Wakuu wa Mikoa kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa viwanda katika maeneo yao ili kuwawezesha wananchi kuongeza thamani ya mazao yao na kuzalisha ajira.

Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 13 Juni, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Waakuu wa Mikoa ya Tanzania Bara, kikao ambacho kimehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Mcheche Masaju, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi na baadhi ya Mawaziri.

Mhe. Rais Magufuli amesema kila Mkuu wa Mkoa anapaswa kufanyia kazi fursa za uanzishaji wa viwanda katika eneo lake na kuhakikisha anashawishi wawekezaji kuzitumia fursa hizo kama inavyofanyika katika Mkoa wa Pwani ambako tangu Awamu ya Tano iingie madarakani viwanda vikubwa 83 vimejengwa na vingine kukamilika huku viwanda vidogo zaidi ya 120 pia vikiwa vimejengwa.

Pamoja na hilo Mhe. Rais Magufuli amewaagiza Wakuu wa Mikoa kuongeza juhudi za utatuzi wa migogoro ya ardhi ikiwa ni pamoja na kuharakisha mchakato wa kuwanyang’anya hati za umiliki wa mashamba makubwa ambayo yanashikiliwa na watu pasipo kuyaendeleza.

“Mashamba yote yaliyotelekezwa, fuateni taratibu za sheria, yanyang’anyeni wapewe Watanzania ambao wapo tayari kuyaendeleza, lakini fanyeni jambo hili kwa kufuata utaratibu” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewatahadharisha Wakuu wa Mikoa hao dhidi ya watu wanaofanya njama za kujimilikisha maeneo makubwa ya ardhi na kusababisha wakulima na wafugaji kukosa maeneo ya kilimo na malisho na ametaka wote watakaobainika kufanya njama hizo wafichuliwe na kunyang’anywa maeneo hayo.

Mhe. Dkt. Magufuli pia amewataka Wakuu wa Mikoa kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji na kuwahimiza wananchi kufanya kazi kwa juhudi na maarifa na kuzalisha chakula cha kutosha katika maeneo yao.

Katika kikao hicho Wakuu wa Mikoa wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa juhudi zake za kuwapigania Watanzania hasa wanyonge na wamemuhakikishia kuwa wataendelea kumuunga mkono katika juhudi hizo ikiwemo kudhibiti wizi wa rasilimali za Taifa kama vile madini na maeneo ya hifadhi za wanyamapori.

Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

0 comments:

Post a Comment

SHARE