WAZIRI
Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imefanikiwa kuokoa Sh bilioni
53.9 kutokana na uchunguzi na operesheni mbalimbali zilizofanywa na
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika mwaka
2016/2017.
Amesema
kiasi hicho cha fedha ni kikubwa mno, ikilinganishwa ni Sh bilioni 7 tu
zilizookolewa katika mwaka 2015/2016. Alisema hayo jana wakati
akifungua semina ya Mtandao wa Wabunge wa Afrika walio katika Mapambano
ya Rushwa (APNAC) Tawi la Tanzania kwenye ukumbi wa African Dream mjini
Dodoma.
Akizungumzia
hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika mapambano dhidi ya
rushwa, alisema Serikali imeanza kupata mrejesho mzuri kwamba watumishi
wa umma wanawajibika ipasavyo na vitendo vya rushwa vinaendelea
kupungua.
“Baadhi
ya hatua tulizochukua ni pamoja na kuimarisha taasisi yetu ya TAKUKURU;
kuimarisha matumizi ya mashine za kielektroniki ili kupunguza mianya ya
kupoteza mapato; kuanzisha mahakama ya mafisadi; kusimamia nidhamu
katika utumishi wa umma na kuchukua hatua za haraka za kinidhamu na za
kisheria dhidi ya watuhumiwa wote wa rushwa na ufisadi,” alisema.
Aliwaomba
wabunge waendelee kuiunga mkono Serikali, kwani haina mzaha kwenye
mapambano hayo. “Serikali haina mzaha kwenye mapambano dhidi ya rushwa
na tutaendelea na mapambano hayo.
Hivyo,
ninaomba waheshimiwa wabunge muendelee kutuunga mkono katika mapambano
haya, twende kwa wananchi tukatoe wito kwao watuunge mkono kwenye vita
hii,” alisisitiza.
“Tayari
tumefanya tathmini na kubaini mianya ya rushwa katika sekta za ardhi,
uchukuzi, biashara na maji na hivyo kuziba mianya hiyo. Tutaendelea
kuiwezesha TAKUKURU ili iendelee na kazi nzuri waliyoianza ya kubaini
mianya na kutoa ushauri wa kuziba mianya hiyo ya rushwa.Lengo letu ni
kuwekeza zaidi kwenye kuzuia, kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba”.
Mapema,
akizungumza katika semina hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
anayeshughulikia Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Angellah Kairuki alisema Takukuru kwa kushirikiana na taasisi zilizo
chini yake, wako njiani kuanzisha mtaala wa somo la rushwa ili
ifundishwe tangu shuleni.
“Napenda
kuwahakikishia waheshimiwa wabunge kwamba Serikali ya awamu ya tano
haitakubali kuona rushwa ikiota mizizi. Tunaamini wanafunzi wakijengewa
uwezo tangu utotoni, watachukia rushwa na hatimaye tutakuwa na Taifa
lenye watu waadilifu,” amesema.
Alisema
kutokana na kazi ya kupunguza watumishi hewa, hadi kufikia Aprili mwaka
huu, Serikali imekwishapokea Sh bilioni 1.2 kwenye akaunti maalumu ya
Takukuru iliyoko Hazina ambazo zinatokana na makusanyo kutoka kwa
waliokuwa watumishi hewa.
Mwakilishi
wa Mkurugenzi Mkazi wa UNDP, Godfrey Mulisa alisema wataendelea
kushirikiana na Bunge katika miradi mbalimbali ikiwemo shughuli
zinazofanywa na APNAC.
Awali,
Mwenyekti wa APNAC tawi la Tanzania, George Mkuchika alisema hadi sasa
wabunge wapatao 148 wamekwishajiunga na mtandao huo. Kwamba anaamini
hadi Bunge hili litakapomaliza muda wake, zaidi ya robo tatu ya wabunge
watakuwa wamejiunga
0 comments:
Post a Comment