Mahakama
Kuu kanda ya Mbeya, kwa kusaidiwa na ushahidi wa baba mzazi wa
mshitakiwa, imemhukumu kunyongwa hadi kufa, Geoffrey Sichizya (27) baada
ya kumtia hatiani kwa kosa la kumua babu yake ili achukue ng’ombe wake
tisa.
Akisoma
hukumu hiyo kwenye Mahakama ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe jana, Jaji
wa Mahakama Kuu Atuganile Ngwala alisema baada ya kusikiliza ushahidi
wa pande zote mbili ameridhika pasipo kuacha shaka kuwa mshitakiwa
alimuua babu yake Labson Sichizya kwa kukusudia.
Alisema
ameridhika na ushahidi uliotolewa na Meas Sichezya ambaye ni baba mzazi
wa mshitakiwa huyo, pamoja na Mashaka Sichizya ambaye ni ndugu wa damu,
ambao kwa pamoja walimkamata siku ya tukio wakiwa na viongozi wa vijiji
na kumpeleka polisi.
Jaji
Ngwala alisema Geofrey kwenye maelezo yake kwa mlinzi wa amani alidai
kuwa alimuua babu yake ili achukue ng’ombe tisa waliokuwa wanamilikiwa
na babu huyo.
Awali,
ilidaiwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Ofmedy Mtenga kwamba
mshitakiwa alimkaba koo babu yake Sichizya hadi kufa Novemba 19, 2012
saa 2:00 asubuhi katika kijiji cha Sakamwela, wilaya ya Mbozi mkoani
Songwe.
Aliendelea
kusema kuwa mshitakiwa huyo baada ya kumuua babu yake huyo kwa kumkaba
koo na kufariki, alimfunga na kamba ya chandarua shingoni na
kumning’niza kwenye mti nyuma ya nyumba yake ili ionekane kama marehemu
alijinyonga.
Mshitakiwa
huyo alikuwa akitetewa na wakili Kamru Habibu, ambaye baada ya hukumu
kutolewa hakuwa na hoja yoyote mbele ya mahakama hiyo.
0 comments:
Post a Comment