Pages

Ads 468x60px

Friday, June 9, 2017

Wasomi, wananchi wapongeza bajeti Kuu ya Serikali 2017/2018

Jovina Bujulu na Benjamin Sawe-MAELEZO
 Baadhi ya wasomi na wananchi wameisifu bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/18 wakisema kuwa imelenga kumkomboa mwananchi na imeakisi ahadi za Rais za kusaidia Tanzania ya uchumi wa viwanda.

Akizungumzia bajeti hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Dk. Benson Bana amesema kuwa bajeti hiyo inajibu maswali mengi yaliyo kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi  na Mpango wa Maendeleo ya Miaka Mitano  2020/21 na Dira ya Taifa  ya Mwaka 2020/25 na kwamba ni yenye kutegua vitendawili vinavyowakabili wananchi katika kujiletea maendeleo.

“Kwa sura ya bajeti ilivyo ni bajeti yenye ukombozi kwa mwananchi wa kawaida kwa sababu inagusa masuala ya kupunguziwa kodi kwenye pembejeo, vyakula, kilimo, miundombinu, umeme na maji,” amesema Dk Bana.

Naye Dk Bashir Ally ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ameipongeza bajeti hiyo na kushauri kuwa baada ya kupitishwa, mchakato wa utekelezaji uanze kwa hamasa ya kisiasa, kitaaluma na kijamii ili kufikia malengo yake.

‘’Unaweza kuwa na mpango mzuri, lakini ikiwa watekelezaji ni wala rushwa, wazembe, na wasiofuata sheria, wala kulipa kodi  ni vigumu kufikia malengo ya bajeti hiyo,’’ alisema Dk. Bashir.

Aliongeza kusema kuwa bajeti hii inajenga msingi wa uchumi wa viwanda kwa kuboresha miundombinu ya reli ya kisasa, bandari, ,  kulinda viwanda vyetu  na kuwekeza kwenye mafunzo ya vijana kutaongeza ari ya kujenga uchumi wa kati na wa viwanda.

Wakati huo huo Mtafiti na Mtaalam wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam Prof. Haji  Semboja alisema  kitendo cha Serikali kuondoa Kodi ya ngezeko la Thamani (VAT) kwa wasafirishaji kutazivutia nchi ambazo hazina bandari kutumia bandari na kuleta kuongeza ajira kwa Watanzania.

Alisema kuondoa kodi ya tozo ya leseni ya barabarani kutairahisishia serikali ukusanyaji wa mapato na gharama  za ukusanyaji wa kodi hizo utakuwa ni mdogo ila akaonya kuwa inaweza kuongeza gharama kwa yule ambaye ataendesha gari mara kwa mara.

Akiongea na Idara ya Habari kwa njia ya simu, Mhadhiri wa ChuoKikuu Huria chaTanzania (OUT) Dkt. Damas Ndumbaro ametaja uwekezaji katika miundombinu, kuondolewa kwa tozo ya kodi ya leseni ya barabarani na punguzo la kodi katika mazao ni mambo muhimu yanayopeleka faraja kwa wananchi na yatachochea maendeleo kwa kiwango kikubwa.

“Karibu asilimia 80 ya watanzania wanaishi vijijini na wanategemea kilimo sasa nafuu ya kodi katika mazao ya kilimo itasaidia sana kuwahamasisha wakulima na kuwainua kiuchumi lakini pia mazao hayo yatatumika katika viwanda mbalimbali ambavyo vinaanzishwa nchini na kuongeza ajira,” alieleza Dkt. Ndumbaro.

Kuhusu kodi ya leseni ya barabarani, Dkt. Ndumbaro alisema kuwa hiyo ni nafuu kubwa kwa watu wenye magari na vyombo vingine vya moto kwani watalipia gharama katika mafuta na hivyo kumfanya mtu alipe kwa kadiri ya anavyotumia chombo chake.

Kwa upande wake Shehe wa Dar es Salaam, Alhaji Musa Salum alisema bajeti hiyo ni ya kizalendo na kimaendeleo kwani imewapa watanzania unafuu na kuwasihi wananchi kuipokea na kuitendea haki kwani imekuja kuboresha maisha yao.

Mmoja wa Wakulima wa Tumbaku na mazao ya chakula, Bw. John Pinini kutoka Tabora ameeleza kufurahishwa na bajeti na kutoa wito kwa Watanzania kuipokea na kuhakikisha wanashirikikatika utekelezaji wakeikiwemo kuhakikisha wanalipa kodi stahili kwa mujibu wa sharia na taratibu.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpanga jana alisoma mapendekezoya bajeti kwa mwaka wa fedha 2017/2018 yenye thamani ya shilingi trilioni 31.7 ambapo miongoni mwa vipaumbele ni pamoja na kuendeleza ukuaji wa uchumi na kujenga uchumi wa kipato cha kati, ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi, kuboresha kilimo cha mazao, mifugo na uvuvi na kuongeza ubora wa elimu, huduma za afya, maji na umeme.

0 comments:

Post a Comment

SHARE