Pages

Ads 468x60px

Wednesday, May 27, 2015

Pinda ajiandikisha Daftari la Kudumu



WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amewataka Watanzania wajiandikishe kwa wingi katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Amesema kwamba, kama watafanikiwa kufanya hivyo, watakuwa na sifa za kuwachagua wagombea wakati wa uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Waziri Mkuu Pinda aliyasema hayo juzi alipokuwa akizungumza baada ya kujiandikisha kwenye ofisi ya Ofisa Mtendaji wa Kata iliyopo Kijiji cha Kibaoni, wilayani Mpanda, Mkoa wa Katavi.

“Ninawasihi Watanzania wote tusiache kutumia fursa hii, kila mtu ahakikishe anajiandikisha kwa sababu ni fursa pekee itakayohakikisha kila mwananchi anashiriki uchaguzi wa kumpata rais, mbunge na diwani katika eneo lake.

“Binafsi nimefarijika kwa kazi inayoendelea hasa hasa katika Halmashauri za Nsimbo na Mlele ambazo zimefanikiwa kuandikisha watu kwa zaidi ya asilimia 100,” alisema Waziri Mkuu Pinda.

Awali akiwasilisha taarifa ya uandikishaji katika Halmashauri ya Mlele, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Godwin Benne, alisema walilenga kuandikisha watu 19,482 lakini hadi kufikia jana walifanikiwa kuandikisha watu 20,292 sawa na asilimia 105.

“Kata ya Kibaoni ambayo ina vituo sita, jana peke yake tuliandikisha watu 1,007 kikiwamo kituo cha Kibaoni ambacho Waziri Mkuu Pinda amejiandikisha,” alisema.

Alivitaja vituo vingine, kuwa ni Milumba, Sungusungu, Ilalangulu, Manga na Shule ya Msingi Kakuni ambako Mama Tunu Pinda alijiandikisha juzi hiyo hiyo.

Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Neneka Rashid, alisema uandikidhaji ulianza Mei 18, mwaka huu kwenye kata 12.

Alisema kwamba hadi kufikia juzi, kata nne zilikuwa zimeandikisha watu 12,001 ambazo ni sawa na asilimia 108.9 ingawa matarajio yao yalikuwa ni kuandikisha watu 11,014.

0 comments:

Post a Comment

SHARE