RAIS
Jakaya Kikwete, amesema Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM),
umegeuka kuwa jukwaa la watu wanaotaka kugombea urais kwa kuwa
makuwadi, mawakala wa kuhonga fedha vijana wenzao badala ya kufanya
mijadala ya kukijenga chama.
Alisema
lazima vijana wa UVCCM wawe wapiganaji, wapambanaji na wanaharakati wa
kukiimarisha chama kwani hatima ya CCM iko mikononi mwao.
Rais
Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, aliyasema hayo Mjini Dodoma
jana wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo
vya Elimu ya Juu nchini.
Alisema
badala ya umoja huo kukaa na kuzungumza mambo ya mustakabali wa chama
na Taifa, baadhi ya viongozi wake huchukua fedha kwa wazee na kuwagawia
vijana.
"Vijana
hampaswi kuwa makuwadi na mawakala wa kuhonga wenzenu, katika Kikao cha
NEC, nilimuita Sixtus Mapunda (Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa) na wenzake
nikamwambia mnakoenda siko rudini huku...sisi tunategemea miaka 30 ijayo
Rais atoke miongoni mwenu hivyo lazima tufanye kazi ya kuwaandaa vijana
ili wawe viongozi wazuri.
"Utakuta
viongozi wanasafirishwa ili kuwasindikiza wazee wanaotaka urais jambo
ambalo haliwezekani vijana kuhusishwa na ugawaji rushwa, enzi zetu hoja
za vijana zilikuwa zina nguvu lakini sasa hivi vijana si tishio tena," alisema.
Aliongeza
kuwa, hivi sasa vijana hawatoi hoja za kukijenga chama hivyo aliwataka
warudishe misingi ya uanzishwaji wake na kusisitiza kuwa, anaamini
shirikisho hilo litakipa uhai CCM na kutoa mawazo ya kujenga chama.
Rais
Kikwete alisema, jukumu la shirikisho hilo ni kukitafutia chama
wanachama, marafiki na kuhakikisha kinaungwa mkono na wanafunzi wa elimu
ya juu na wengine.
"Shirikisho
hili lina wajibu wa kuwa chombo cha uwakilishi wa masilahi ya
wanafunzi, kuwa wepesi kuyatambua mambo yenye masilahi kwa wanafunzi na
kuyasemea.
"Muwe
tumaini na kimbilio la wanafunzi, tatueni changamoto na kuzisemea kwa
chama na Serikali badala ya kuacha mambo yakaharibika...shirikisho hili
ni tanuru la kupika viongozi wa baadaye hivyo lazima muwe na mipango
madhubuti," alisema.
Aliwataka
kuchagua viongozi wazuri, waaminifu, waadilifu, wabunifu na wachapa
kazi ndani ya shirikisho ambao watakuwa na uwezo wa kujenga hoja.
"Chama kinasema jitokezeni kugombea, nasubiri hiyo Juni 3, mwaka huu nione watajitokeza wangapi maana ninavyosikia
wako wengi zaidi ya 20 wanaotaka urais.
"Lazima
tushirikiane kujenga chama chetu na shirikisho, mimi nilijaribu mwaka
1995 kugombea urais lakini kura hazikutosha na sikumnunia Mzee Mkapa," alisema Rais Kikwete.
Awali,
akimkaribisha mgeni rasmi, mlezi wa shirikisho hilo Bw.January Makamba,
alisema shirikisho lina matawi 137 katika mikoa mbalimbali nchini
ambapo changamoto zinazowakabili vijana ni mikopo ya wanafunzi,
ushirikishwaji katika kampeni na suala la ajira hivyo alimwomba Rais
Kikwete kuyatafutia ufumbuzi.
0 comments:
Post a Comment