Pages

Ads 468x60px

Saturday, June 27, 2015

Kikwete >> Vita Dhidi ya Madawa ya Kulevya ni Ngumu -


Rais Kikwete amewaongoza watanzania katika maadhimisho ya siku ya kupinga matumizi ya dawa za kulevya duniani yaliyofanyika kitaifa mjini Bagamoyo katika viwanja vya shule ya msingi Mwanamakuka.

Shughuli hizo zilianza kwa maandamano katika viwanja hivyo ambapo badaye mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alimkaribisha Rais pamoja na wananchi waliohudhuria katika viwanja hivyo.

Katika hotuba yake, Rais Jakaya kikwete alisema vita dhidi ya madawa ya kulevya ni kubwa na inahusisha wafanyabiashara wakubwa ambapo fedha zinazopatikana hutumika kufadhili uhalifu wa kimataifa ikiwemo ugaidi.

Rais Kikwete alisema anajivunia kutungwa kwa sheria mpya ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya ya mwaka 2015 katika serikali ya awamu ya nne, ambayo inaweka masharti ya kuundwa kwa chombo maalum kitakachoshughulikia kwa ukaribu tatizo hilo, na kwamba anataka chombo hicho kiwe kimeundwa kabla ya Oktoba ili kutoa baraka zake kabla hajaondoka madarakani, na atamkabidhi Rais ajaye aendelee kuanzia hapo.

Awali Waziri wa Afya na ustawi wa jamii, Dkt Seif Rashid alipata fursa ya kufafanua mikakati ya serikali katika kupambana na tatizo la matumizi ya madawa ya kulevya na kuwapiga vita wafanyabiashara wanaojihusisha na dawa hizo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi isiyokuwa ya serikali inayojishughulisha na masuala ya vijana Tanzania Youth Aliance TAYOA, Peter Masika alisema kwamba wamezindua namba ya simu itakayotumika kuwaelimisha vijana dhidi ya athari ya matumizi ya madawa ya kulevya.

Wakati huo huo mwanaharakati anayepambana na matumizi ya madawa ya kulevya Rehema Chalamila – Ray C aliwataka vijana wenzake waliojitumbukiza katika janga hili waweze kufuata mfano wake na wajitokeze kutokomeza janga hili kwa kutumia dawa za Methadoni na kuacha kabisa madawa.

Katika maadhimisho hayo ambayo yaliyoongozwa na kauli mbiu ya tujenge jamii na maisha ya utu bila dawa za kulevya, Rais kikwete alihimiza ushirikiano kwa jamii katika kupinga matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana na kutokomeza biashara hiyo ikiwemo utoaji wa elimu ya kutosha kwa jamii ili kuwasaidia vijana walioathirika na dawa za kulevya.

0 comments:

Post a Comment

SHARE