WAZIRI Mkuu mstaafu Edward Lowassa amesema huenda akamzuia Mbunge wa
Jimbo la Kigoma, Peter Serukamba kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa
Oktoba mwaka huu ili amsaidie jukumu muhimu kwenye safari yake ya
matumaini.
Akizungumza wakati wa kuomba udhamini kutoka kwa wanachama wa CCM
mkoa Kigoma katika ofisi kuu ya CCM mkoa, Lowassa alisema Serukamba ni
mmoja wa wanakamati katika safari hiyo ya matumaini.
Lowassa, anayewania kuteuliwa kugombea Urais wa Tanzania kwa tiketi
ya CCM alisema katika safari hiyo kama mwanakamati Serukamba anayo
majukumu muhimu ambayo anapaswa ayatekeleze zaidi ya kugombea ubunge.
“Ndugu zangu wananchi wa Kigoma nimekumbuka jambo moja ninaye mwana
kamati ambaye ni mtoto wenu hapa Kigoma, Mbunge wenu Serukamba, yeye ni
mmoja wa wajumbe katika kamati yangu alikuwa na dhamira ya kugombea tena
ubunge, lakini mnaweza msimuone maana atakuwa na majukumu makubwa ya
kunisaidia kwenye kamati,” alisema Lowassa.
Pamoja na kutogombea ubunge kiongozi huyo alisema Serukamba anayo
dhamira ya dhati katika kuwatumikia wananchi wa mkoa Kigoma na ili
kutimiza lengo hilo ameomba wasali na kumuombea sana ili aweze
kupitishwa na chama chake kugombea Urais, lakini pia kushinda katika
uchaguzi mkuu.
Serukamba ambaye kwa sasa anamaliza muhula wake kama Mbunge wa Jimbo
la Kigoma Mjini anatarajia kugombea tena ubunge katika jimbo la Kigoma
Kaskazini.
0 comments:
Post a Comment