Pages

Ads 468x60px

Monday, June 15, 2015

URAIS:::> Mgombea Urais wa ACT-Wazalendo Kujulikana Agosti 10



MGOMBEA wa Urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu kupitia chama cha ACT-Wazalendo, anatarajia kujulikana Agosti 10 mwaka huu.
 
Atakayebahatika kupeperusha bendera ya ACT-Wazalendo pia atawajibika kuwa tayari kutangaza mali binafsi na vyanzo vyake kwa kutokana na utaratibu ulioainishwa katika sehemu ya sita ya nyongeza ya kwanza ya Katiba ya Chama hicho.
 
Hayo yalisemwa jana mjini Geita na kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, wakati akihutubia wananchi mjini humo. Zitto alisema Halmashauri kuu ya chama hicho iliyokutana juzi mjini Tabora, pia imepitisha ratiba kamili ya kuchukua na kurudisha fomu kwa nafasi mbali mbali za chama hicho kuanzia Julai mosi.
 
Alisema kuanzia Julai mosi mpaka Julai 17 itakuwa ni siku ya kuchukua fomu kwa ngazi ya udiwani kwa ada ya Sh 10,000, Julai 1-26 kwa ngazi ya Ubunge na uwakilishi na ada yake ni Sh 20,000 na kwa ngazi ya urais ni kuanzia Julai 1-26 na ada yake ni Sh 100,000.
 
Aliongeza kuwa vikao vya ngazi mbali mbali ya uteuzi vitaanza Julai 27 mpaka siku ya mwisho ya Agosti 10 wakati mkutano mkuu wa Chama utakapopitisha jina la mgombea Urais.
 
“Kwa nafasi ya urais mtu anayetaka kutuwakilisha kupitia ACT-Wazalendo ni lazima awe amethibitika kuielewa itikadi, falsafa, misingi na sera za ACT-Wazalendo na aoneshe utayari wa kuisimamia na kuishi awe ni mtu anayejitegemea kutokana na chanzo halali cha kipato kutokana na shughuli halali.”
 
Sifa zingine alizotaja kwa nafasi hiyo ni pamoja na mwombaji kuwa ni mtu anayeonesha kuyaelewa matatizo ya Tanzania ya sasa na ya muda mrefu, na mwenye maono mapana juu ya maendeleo ya Tanzania ya sasa na ya kizazi kijacho, awe na upeo mpana kuhusu masuala ya Afrika na ulimwengu katika nyanja za kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni, kijiografia na kijamii.

0 comments:

Post a Comment

SHARE