Pages

Ads 468x60px

Monday, June 15, 2015

Rais Obama Kupelekewa ‘kifimbo’ cha Nyerere>>SOMA HAPA



RAIS wa Marekani, Barack Obama anatarajiwa kuwa kiongozi wa tatu duniani kuanza kubeba kifimbo kama kile cha Mwalimu Nyerere ambacho tayari kimechongwa kwa ajili yake na msanii yule yule aliyetengeneza fimbo ya Baba wa Taifa.
 
Kiongozi wa pili kukabidhiwa ‘kifimbo cha uongozi,’ kama kile cha Nyerere alikuwa ni Rais Jakaya Kikwete aliyepewa rasmi fimbo yake mwishoni mwa wiki mjini Arusha, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Albino Duniani iliyofanyika kitaifa mjini hapa. Kikwete ndiye aliyekuwa mgeni rasmi.
 
Kifimbo cha kwanza cha Mwalimu Nyerere kilichongwa mwanzoni kabisa mwa miaka ya 1960 na mtaalamu wa sanaa za uchoraji, uchongaji na sayansi za kitamaduni, Athuman Omari Mwariko, ambaye pia ndiye aliyeisanifu ngao ya taifa pamoja na mwenge wa amani duniani.
 
“Nilimchongea tena Mwalimu Nyerere Kifimbo cha Pili mnamo mwaka 1985 kipindi kifupi tu kabla hajastaafu rasmi kutoka Ikulu,” anasema Mwariko na inaonekana pia ameamua kuchonga kifimbo cha tatu na kumkabidhi Rais Kikwete kabla kiongozi huyo hajang’atuka madarakani Oktoba mwaka huu.
 
Katika maisha yake yote, Mwaruko amechonga fimbo nne tu za uongozi na waliobahatika kuvibeba vifimbo hivyo maalumu hadi sasa ni Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, Rais Jakaya Kikwete na hivi karibuni sasa itakuwa ni Rais Barack Obama wa Marekani.
 
“Nimekwisha kupeleka ujumbe maalumu kwa Rais Obama pamoja na Ikulu ya Marekani ili waandae siku na sehemu maalumu ambayo nitakwenda na kumkabidhi rasmi kiongozi huyo fimbo maalumu ya uongozi,” alisema Mwaruko ambaye pia amekuwa akiishi na kufanya kazi nchini Marekani kwa miaka mingi.
 
Kuhusu fimbo ya Mwalimu Nyerere, Mwariko anasema; “Kila kiongozi ni sharti awe na fimbo ya kuongozea,” anaongeza kuwa alimtengenezea Nyerere fimbo yake ya kwanza wakati akianza uongozi miaka ya 1960 na baadaye kumkabidhi fimbo ya pili wakati kiongozi huyo akistaafu urais mwaka 1985.
 
“Mimi ndiye nina siri ya mti uliotumika kuchongea fimbo hizo,” anasema Mwariko na kuongeza kuwa fimbo zote za Mwalimu zilikuwa za kawaida tu na wala hazina nguvu za ziada au miujiza kama watu wanavyozusha.
 
Makazi yake nchini kwa sasa ni katika eneo la Njoro, katikati ya Pasua na Majengo, wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro, akasema atakuwepo hadi baada ya uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu.
 
Mzee Mwariko alizaliwa mwaka 1949 eneo la Mbuyuni wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro na alihudhuria masomo ya Msingi Handeni, Tanga na baadae Moshi kabla ya kujiunga na Kings College ya Uganda na baadaye Chuo Kikuu Cha Makerere nchini humo.
 
Mafunzo mengine aliyapata katika Chuo cha Sanaa cha Potopoto cha Congo Brazaville, Chuo cha Lincoln, Uingereza na Chuo Kikuu Cha Havard, Marekani. Mwariko ndiye mchoraji pekee kutoka Afrika aliyeshinda tuzo katika mashindano ya nchini Brazil mwaka 1986.

0 comments:

Post a Comment

SHARE