Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Serikali
kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imeahidi kuendelea kusimamia na
kufuatilia sheria na miongozo yote iliyotolewa ili kuhakikisha lengo la
kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima kwenye Mashirika na Taasisi za Umma
ikiwemo safari za nje na posho za wajumbe wa Bodi za mashirika na
Taasisi zote za Umma linafanikiwa.
Hayo
yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,
Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Vwawa
(CCM), Mhe. Japhet Hasunga ambaye alitaka kujua hatua ambazo Serikali
inatarajia kuchukua kudhibiti matumizi ya fedha za Umma katika Taasisi
zake.
Dkt.
Kijaji alisema kuwa Serikali imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa
matumizi ya fedha za Umma yasiyo ya lazima yanadhibitiwa kikamilifu
kupitia Sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge ikiwemo Sheria ya Bajeti
Na. 11 ya mwaka 2015 ambayo imebainishwa hatua mbalimbali za kibajeti
zenye lengo la kuongeza usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za
Umma katika Mashirika na Taasisi za Umma.
“Sheria
hiyo imebainisha utolewaji wa Mwongozo wa Mipango na Bajeti wa Serikali
unaojumuisha Mashirika na Taasisi zote za Serikali ambao unatoa
miongozo mbalimbali ya kuzingatiwa katika matumizi ya Umma kwa mwaka
husika,” alifafanua Dkt. Kijaji
Alisema
kuwa kupitia Sheria hiyo, Ofisi ya Msajili wa Hazina imepewa mamlaka ya
kupitia bajeti za Mashirika na Taasisi zilizo chini yake kwa kuzingatia
miongozo na mipango ya Serikali inayotarajiwa kutekelezwa.
Mhe.
Kijaji alibainisha kuwa katika Sheria hiyo Ofisi ya Msajili wa Hazina
imepewa jukumu la kupitia na kuridhia kanuni za fedha za Mashirika na
Taasisi zote za Umma ili kuimarisha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya
fedha za Umma.
“Sheria
nyingine iliyopitishwa na Bunge ni marekebisho ya Sheria ya Fedha ya
Mwaka 2015 ambayo iliweka ukomo kwa Taasisi na Mashirika ya Umma kutumia
asilimia 60 tu ya mapato yake kwa matumizi ya kawaida yasiyojumuisha
mishahara,” aliongeza Dkt. Kijaji.
Aidha,
Dkt. Kijaji alisema kuwa katika kuhakikisha Ofisi ya Msajili wa Hazina
inatekeleza majukumu yake kisheria, imetoa miongozo mbalimbali yenye
lengo la kudhibiti matumizi ya Mashirika na Taasisi za Umma ili
kupunguza matumizi ya Serikali yasiyo ya lazima.
“Miongoni
mwa miongozo hiyo ni barua iliyotolewa na Msajili wa Hazina tarehe 10
Novemba, 2015 ya kudhibiti safari za nje ya nchi zisizo za lazima kwa
watumishi wa Mashirika na Taasisi za Umma ambazo awali zilionekana
kutumia sehemu kubwa ya fedha za Umma,” alisema Dkt. Kijaji.
Aliongeza
kuwa waraka wa Msajili wa Hazina Na. 12 wa mwaka 2015 kuhusu Posho za
Vikao vya Bodi ya Wakurugenzi wa Mashirika na Taasisi za Umma pia ni
miongoni mwa miongozo ya kuzuia matumizi yasiyo ya lazima kwani waraka
huo umefuta posho za vikao vya Bodi na kuondoa utaratibu wa Bodi kuwa na
vikao zaidi ya vinne kwa mwaka.
Dkt.
Kijaji alisema kuwa Waraka wa Msajili wa Hazina Na. 1 wa mwaka 2016
kuhusu posho za kujikimu kwa Wajumbe wa Bodi za Wakurugenzi wa Mashirika
na Taasisi za Umma ulikuwa na lengo la kuendeleza jitihada za Serikali
kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya fedha za Umma.
Alisema
kuwa Waraka huo uliweka ukomo wa posho hizo kwa Wajumbe wa Bodi kwa
safari za ndani na nje ya nchi, huku akisisitiza kuwa bado Serikali
itaendelea kuhakikisha matumizi ya fedha za Umma yasiyo ya lazima
yanadhibitiwa kikamilifu.
0 comments:
Post a Comment