Pages

Ads 468x60px

Tuesday, June 13, 2017

Waziri Mkuu Majaliwa awavalisha vyeo Maafisa wa Magereza, ahimiza haki na usawa

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka maaafisa na makamanda wa Jeshi la Magereza nchini waendelee kusimamia haki na usawa wanapotimiza wajibu wao.

Majaliwa amesema hayo wakati akizungumza na maafisa na makamanda wa jeshi hilo katika hafla ya kuwavisha vyeo maafisa 29 iliyofanyika kwenye viwanja vya Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCTA), Ukonga, jijini Dar es Salaam.

Akifanya kazi hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, amewavisha vyeo maafisa watano kuwa Naibu Kamishna wa Magereza (DCP) na maafisa 24 kuwa Kamishna Waandamizi Wasaidizi wa Magereza (SACP). Maaafisa hao walipandishwa vyeo Mei 25, mwaka huu.

“Ninyi ni viongozi wakuu katika mikoa mnayotoka. Huko kuna makamanda walio chini yenu na jamii inayowazunguka. Endeleeni kuwahudumiana na kulitumikia Taifa hili kwa weledi mkubwa. Endeleeni kusimamia usawa na haki katika kazi zenu za kila siku,” amesema.

Majaliwa amesema hana shaka na utendaji kazi wa jeshi la Magereza kwani watumishi wake ni waadilifu. “Jeshi hili linayo nidhamu ya hali ya juu, mbali ya jukumu lenu la ulinzi, mnafanya kazi nidhamu, weledi na uadilifu mkubwa,” amesema.

Amesema Serikali inatambua changamoto zinazowakabili katika utendaji wao wa kila siku na kwamba inajitahidi kuzishughulikia hasa baada ya kukamilisha zoezi la kuondoa watumishi hewa.

0 comments:

Post a Comment

SHARE