Pages

Ads 468x60px

Friday, May 29, 2015

Tanzania Kuendelea Kupokea Wakimbizi wa Burundi



TANZANIA imetangaza kuendelea kupokea wakimbizi wanaoingia nchini kutoka Burundi kutokana na kuendelea kwa machafuko nchini humo huku waandamanaji wakipambana na polisi kupinga hatua ya Rais Pierre Nkurunzinza kugombea urais kwa muhula wa tatu.
 
Akizungumza  katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kabla ya kuanza safari ya kukagua kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu Wilayani Kasulu jana, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe alisema uamuzi huo unalenga kutoa nafasi ya wakimbizi hao kupata mahitaji ya msingi.
 
Waziri Chikawe alisema wakimbizi wana haki ya kulindwa na kuthaminiwa kama raia wengine kwa hivyo uamuzi wa Serikali kutoa nafasi zaidi kwa wakimbizi nchini una nia ya kutoa nafasi zaidi ili kupata mahitaji yao ya msingi ikiwa ni pamoja na misaada mbalimbali ya binadamu kupitia mashirika mbalimbali.
 
 “Kama nchi tumeona ni vema kuendelea kuwapokea, hivyo tumetoa nafasi ya kuendelea kuwapokea wakimbizi hawa kutoka nchini Burundi mpaka hapo hali ya usalama nchini mwao itakapoimarika,” alisema Chikawe.
 
Waziri Chikawe pia aliyaomba mashirika mbalimbali ya kimataifa kusaidia wakimbizi hao wanaoendelea kumiminika nchini kwa wingi kusaidiana na serikali ili kuwapa huduma za malazi na chakula.
 
  Mratibu Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Alvaro Rodriguez alisema mpaka sasa hali ya siasa  Burundi inatia shaka kwa kuwa inaweza kusababisha ongezeko kubwa la wakimbizi Tanzania.
 
Alisema Tanzania ni nchi ya mfano wa kuigwa kwa namna inavyoshughulikia wakimbizi ikiwa ni pamoja na kuwapokea hiyvo umoja wa mataifa unaungana na nia ya Serikali ya Tanzania kuwasaidia wakimbizi hao.
 
Alisema kutokana na kuendelea kupokea idadi kubwa ya wakimbizi, kambi ya Nyarugusu imeendelea kuelemewa na wakimbizi hivyo kuliomba shirika la Umoja wa Mataifa kusaidia uwezekano wa kuongeza kambi nyingine kwa ajili ya wakimbizi hao.

0 comments:

Post a Comment

SHARE