Mbio za kusaka urais kwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimezidi
kushika kasi baada ya mtoto wa tano wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu
Nyerere, Charles Makongoro Nyerere kujitosa kwenye kinyang’anyiro hicho.
Wakati Makongoro akichukua uamuzi huo kwa mara ya kwanza katika historia
ya familia ya Mwalimu Nyerere, mkoani Mbeya Waziri wa Nchi,Ofisi ya
Rais Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya naye ameingia kwenye mbio
hizo.
Makongoro
Akitangaza nia yake katika eneo la Mwitongo kijijini Butiama jana,
Makongoro aliwashambulia makada wenzake ndani ya CCM ambao wanaongoza
makundi ya kuwania urais kwa kuwaita ni ‘vibaka’ wanaokivuruga chama
hicho kwa maslahi yao binafsi.
Akitoa mfano kwa baadhi ya makada wanaoongoza makundi ndani ya chama
hicho, Makongoro aliwataja kwa majina kuwa ni Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Naibu Waziri wa
Fedha,Mwigulu Nchemba na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven
Wasira.
Alisema makada hao kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia fedha nyingi
kuendesha makundi ya urais na akahoji sababu za kutafuta cheo hicho cha
juu kwa fedha.
"CCM irudishwe kwa wazalendo kwa sababu vibaka wamekuwa na mlengo mbaya wa kukiendeleza chama hicho," alisema.
Alisema ndani ya chama hicho kumekuwa maradhi ya rushwa ambayo yameiambukiza nchi nzima.
Makongoro alisema yeye ni mzalendo wa kweli na anataka kuirudisha nchi
katika misingi ya uadilifu endapo CCM itampa ridhaa ya kupeperusha
bendera katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Alisema ndani ya chama hicho kumekuibuka genge la watu wachache ambao utajiri wao ni wa shaka na umejijenga kwa fedha chafu.
“Ndani ya chama tawala wamekuwapo ‘vibaka’ wachache… unajua kibaka ni
kibaka tu hata kama kapewa gari la Serikali lina bendera ya taifa mbele
atabaki kuwa kibaka tu.
“Wananijua vizuri huwa siwaonei haya kuwaambia ukweli, hawa ndiyo
wanaotuvurugia chama na hawamheshimu Mwenyekiti wa chama, Rais Jakaya
Kikwete,” alisema Makongoro.
Katika hotuba yake ambayo alitumia saa mbili, Makongoro alijikita kuzungumzia madhara yanayotokana na rushwa ndani ya CCM.
Alisema baadhi ya makada wanaotumia rushwa wamezalisha makundi na
mipasuko isiyo ya lazima huku akisisitiza kuwa anachukia kuwapo makundi
ndani ya chama hicho.
Kwa mujibu wa Makongoro, hali hiyo imechochea badhi ya viongozi wa CCM
katika ngazi mbalimbali wakiwamo wenyeviti wa mikoa na wajumbe wa
Halmashauri Kuu ya chama hicho kuishi kama mifugo.
Alisema hali hiyo imesababisha baadhi ya viongozi hao kuishi maisha ya
kusukumwa kwa upepo wa makundi yanayomilikiwa na watoa fedha.
“Vibaka waturudishie CCM yetu, watambue wao ni wachache na sisi wazalendo ni wengi, hawatushindi na fedha zao na kitaeleweka tu.
“Leo hii viongozi wetu wa CCM wamekuwa ni watu wa kuendeshwa na vibaka
hawa wanahongwa fedha ovyo…wao wana mifugo yao ndani ya NEC basi mimi
sijafuga hata kuku, nasema kitaweleweka,” alisema Makongoro.
Alisema yeye hawezi kufanya hivyo kwa sababu rasimu ya ilani ya chama
hicho bado haijapitishwa na chama, hofu yake ni kwamba anaweza kutoa
ahadi na zikawa kinyuume na ilani ya chama chake.
“Nimewasikia wanajinadi,nawashangaa sana, najiuliza kwani wao ni akina
nani watoe ahadi kabla ya ilani ya chama? Ikitokea ahadi yako ikaenda
kinyume na ilani si ndiyo mwanzo wa kuwa na rais muongo…sitaki kuwa rais
muongo nitaheshimu chama changu kwa kila mchakato na maelekezo,”
alisema Makongoro.
Aliwaasa Watanzania wawaogope watu wanaoonekana kuwa na haraka ya kukimbilia kutawala nchi.
“Ukiona watu kazi inatangazwa ifanywe kwa utaratibu wake na mtu
aliyeiomba kazi hiyo anakiuka taratibu, muogopeni sana huyo hafai
kukukuongoza maana hata akikuongoza ataendelea kukiuka taratibu ili
ajinufaishe,” alisema Makongoro.
Wanawake wananipenda
Makongoro alisema anakerwa na siasa chafu dhidi yake zinazoenezwa na baadhi ya wanasiasa wenzake ndani ya CCM.
Alizitaja siasa hizo kuwa ni tuhuma za kulaaniwa na baba yake, ulevi na mtu anayependa wanawake.
Akijibu tuhuma hizo, Makongoro alihoji umati uliomiminika kumsikiliza
kwamba, “jamani naonekana nimelaaniwa? Naelekea kuokota makopo? Jamani
mnanionaje, naonekana mlevi? na umati ulikataa kwa kusema, “hapana”.
“Eti wanasema Makongoro anapenda wanawake sasa wanataka nipende wanaume?
Wanawake wananipenda na mimi nawapenda, hizi siasa chafu wanazonituhumu
hazinisumbuilangu ni moja tu vibaka rudisheni nchi yetu,” alisema.
Nimrod Mkono
Naye Mbunge wa Musoma Vijijini , Nimrode Mkono alisema atakuwa bega
kwa bega na Makongoro kuanzia sasa katika safari yake ya kuwania urais
mpaka hatua ya mwisho.
“Wapo wengi walionifuata niwe nao katika harakati zao za kuwania urais,
sasa nawaambia ‘bye bye’ nipo na Makongoro na wasijihangaishe
kunitafuta,” alisema Mkono.
Shyrose
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashari, Shyrose Banji na mwanamuziki wa
kizazi kipya, Judith Wambura ‘Lady J Dee’ nao walihudhuria kikao hicho.
Makongoro afananishwa na Daudi
Awali kabla ya Makongoro kutangaza nia ya kugombea urais,baadhi ya
viongozi wa dini walimuombea ambako Mchungaji wa Kanisa la Anglikana,
Jackob Ngagani alimfananisha na Daudi.
Alisema anaamini Mungu atamuongoza Makongoro kushinda ushindani wa kupata mgombea urais kupitia CCM.
Kabla ya dua ya viongozi wa dini, wazee wa kabila la Wazanaki,
walimvisha vazi la asili la kabila hilo na kumkabidhi fimbo kwa ajili ya
kuwaongoza Watanzania.
Naye Chifu wa Kabila la Wazanaki, Japhet Wanzagi alisema Makongoro ni simba na kusisitiza kuwa kabila lao huwa halibahatishi.
0 comments:
Post a Comment