Kufuatia
taarifa zilizokuwa zikienea na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii,
zikidai kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limewatelekeza
wachezaji wa timu ya mpira wa miguu ya Tanzania ya vijana wenye umri wa
chini ya miaka 17(Serengeti Boys), TFF imejitokeza na kukanusha taarifa
hizo.
Taarifa
hizo za uongo zilidai kuwa Serengeti Boys hawakulipwa posho na
kushutumu viongozi wa juu wa shirikisho kuhusu jambo hilo.
“Tunapenda
kuwajulisha wazazi na umma kwa ujumla kwamba vijana wetu walilipwa
posho zao zote wakiwa kambini Morocco na Cameroon na zile za mashindano
ya AFCON nchini Gabon.” wamesema TFF
Kwa
mujibu wa Taarifa kutoka TFF, zimeeleza kuwa Shirikisho linafanya
taratibu za kupeleka maombi kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu
(Football Development Fund FDF) ili kuweza kuwalipa vijana na benchi la
ufundi sehemu ya posho zilizokuwa bado hazijakamilishwa wakati wa
michuano ya kufuzu kwa AFCON 2017.
“Tumeshtushwa
na taarifa hizo ambazo tafsiri yake ni kuharibu uhusiano mwema kati ya
shirikisho, wazazi na wachezaji ambao wanatarajiwa kuitumikia timu ya
Taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 maarufu kama Ngorongoro
Heroes.”
TFF
wamesema kuwa wanawatambua vijana wa Serengeti Boys kwani bado ni
sehemu ya kikosi cha Ngorongoro Heroes na hivyo ukifika wakati wataitwa
kambini kwa ajili ya michezo ya kimataifa ya U-20.
Aidha,
Wametoa shukrani kwa kuushukuru umma ambao wameendelea kuchangia Mfuko
wa FDF ambao kimsingi kazi yake ni kutafuta rasilimali kwa ajili ya
maendeleo ya mpira.
“Tunaomba
michango iendelee kwani bado tuna changamoto za mashindano mbalimbali
kwa timu za wanawake na vijana ikiwemo fainali za wanawake Afrika
zitakazofanyika Ghana hapo mwakani kwa timu ya Twiga Stars na AFCON 2019
kwa Serengeti Boys ambayo itakuwa mwenyeji.”
Mfuko
wa Maendeleo ya Mpira – FDF ulianzishwa kwa lengo la kutafuta
rasilimali za maendeleo ya mpira wa miguu hasa kwa wanawake na vijana
pamoja na miundombinu ya mchezo huo.
0 comments:
Post a Comment