Pages

Ads 468x60px

Thursday, May 28, 2015

Spika Makinda: Bangi ya Njombe si kali


SPIKA wa Bunge, Anne Makinda amesema, bangi inayolimwa katika Mkoa wa Njombe si kali kama inayolimwa mikoa mingine kutokana na baridi iliyopo mkoani humo.
Makinda alijikuta akitoa jibu hilo huku akicheka kutokana na swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Christowaja Mtinda (Chadema), ambaye alisema kuna baadhi ya maeneo nchini ukiwemo Mkoa wa Njombe na Mara, mmea wa bangi umekuwa ukiota bila kupandwa na hutumika kama chakula.
 

“Njombe bangi haioti yenyewe, tulikuwa tunapanda, lakini baada ya sheria iliyopitishwa mwaka 1975, tuliacha kupanda bangi, lakini hata hivyo bangi ya Njombe si kali kwa sababu ya baridi,” alisema Spika Makinda huku akiwaacha wabunge na wageni wengine wakicheka.
Katika swali hilo, Mtinda aliitaka Serikali kufanya utafiti ili mmea huo uweze kutumika kama dawa.
Hata hivyo, akijibu kwa Niaba ya Waziri wa Afya, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia alisema Serikali haipo tayari kuhalalisha matumizi ya bangi kama dawa kwa sababu athari zake ni nyingi kuliko faida.


Awali, katika swali la msingi Mbunge wa Viti Maalumu, Leticia Nyerere (Chadema), alitaka kujua kuhusu msimamo wa Serikali kuhalalisha matumzi ya bangi kama dawa kama ilivyofanya Serikali ya Columbia iliyoruhusu matumizi ya bangi kwa ajili ya dawa.
Akijibu Nkamia alisema, msimamo wa Serikali ni kwamba inafuata sheria inayoeleza kwa kina mtu yeyote atakayejihusisha na kutumia, kuhamasisha matumizi, kuuza, kusafirisha, kuhifadhi au kujihusisha kwa namna yoyote ile na bangi ni kosa la jinai.
“Adhabu ya makosa hayo ni kufikia hadi kifungo cha maisha. 


Napenda kushauri na kusisitiza bangi ni miongoni mwa dawa za kulevya ambazo tusizizalishe wala kuzisambaza kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa afya ya binadamu,” alisema Nkamia.

0 comments:

Post a Comment

SHARE