ASKOFU
wa Jimbo Katoliki la Rulenge –Ngara, Severine Niwemugizi, amesema
anaunga mkono azma ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ya
kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana.
Sambamba
na hilo, amewataka Watanzania kumwomba Mwenyezi Mungu ili awawezeshe
kuchagua kiongozi bora na kuonya kauli yake isichukuliwe kuwa ni
kumpigia kampeni Lowassa katika safari yake ya matumaini.
Akizungumza
jana katika jubilee ya miaka 50 ya Seminari ndogo ya Mt. Karoli Lwanga
iliyoko Katoke wilayani Biharamulo, Askofu Niwemugizi alisema alianza
kumuunga mkono Lowassa katika azma yake ya kukabiliana na tatizo la
ajira kwa vijana tangu alipokuwa Waziri Mkuu mwaka 2007.
“Tuiombee
nchi yetu ipate viongozi makini, waadilifu na wakweli watakaoongoza
nchi kwa misingi ya haki na usawa, ambao watajenga jamii yenye
kuaminiana na kuheshimiana inayojali mema ya wote, watakaolinda na
kudumisha umoja wa taifa.
“Najua
wewe ndiye muasisi wa shule za kata, sasa zina wanafunzi wengi sana,
lakini wanapomaliza kidato cha nne wengi wao wanarudi vijijini na
wanajikuta wakikosa ajira. Hii inawatesa sana na wana hasira. Naungana
nawe katika kukabili changamoto za vijana ambayo umekuwa ukiizungumzia
sana,” alisema Askofu Niwemugizi.
Kiongozi
huyo wa kanisa pia alimshukuru Lowassa kwa msaada alioutoa wa kutatua
mgogoro wa ardhi wa Two Two wilayani Biharamulo wakati akiwa Waziri Mkuu
mwaka 2007.
Alisema
Lowassa alifika Chato mwaka 2007 na kuzungumza na wananchi katika
mkutano wa hadhara na yeye alimwomba asaidie kutatua changamoto ya
ardhi.
“Ulimwagiza aliyekuwa Waziri wa Ardhi wakati huo, John Magufuli ashughulikie kadhia hiyo na akueleze ardhi hiyo ni ya nani,” alisema Niwemugizi.
Akizungumzia
mkakati alionao wa kuunga mkono azma ya Lowassa ya kukabiliana na
tatizo la ajira, Askofu Niwemugizi alisema atalitumia eneo hilo kujenga
chuo kikuu cha kufundisha ufundi stadi na ujasiriamali.
“Inaweza
kuchukua muda mrefu, lakini hii ni azma yetu. Lengo ni kuhakikisha
shule zetu zote jimboni zinatoa elimu ya ufundi pamoja na masomo mengine
na watakaofaulu waendelee kupata elimu ya juu ya ufundi stadi ili
wajiajiri na kuajiri wengine,” alisema.
Awali
Askofu Niwemugizi alieleza kuwa jubilee hiyo ilipangwa kufanyika mwaka
jana, lakini mgeni rasmi aliyekusudiwa kuwapo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda
hakupatikana hivyo waliamua kuifanya mwaka huu.
“Ninafurahi
na kumshukuru sana Edward Lowassa kukubali mwaliko wangu, tena katika
taarifa ya muda mfupi tu akakubali kuja kuwa nasi leo, watu wanaweza
kufikiri nimekuita kukupigia kampeni katika safari yako ya matumaini
uliyoitangaza kule Arusha Jumamosi Mei 30, watakaotaka kuliona hilo ni
juu yao, lakini nafikiri tuna uhuru wa kuchagua,” alisema.
Naye
Lowassa alipopewa fursa ya kuzungumza, alisema anaomba sala kutoka kwa
Watanzania ili Mungu akijalia katika safari yake ya matumaini kazi yake
ya kwanza iwe kuunda chombo maalumu kitakachowashirikisha wadau na
wataalamu wa elimu.
Alisema
chombo hicho kitapitia mfumo wa elimu kuanzia elimu ya awali, msingi,
sekondari, ufundi na vyuo vikuu ili kupata mwongozo thabiti.
“Naamini
hamna wasiwasi na usimamizi wangu katika kufanikisha utekelezaji wa
mambo ya msingi ya nchi, umefika wakati wa nchi yetu kujibu kwanza
swali, tunataka kujenga taifa gani, nini mwelekeo wetu kama taifa
kiuchumi, kisiasa na kijamii.
“Pamoja
na yote uliyosema Baba Askofu, umeeleza matatizo ya elimu kwa ufasaha
mkubwa, nami nakubaliana nawe, umefika wakati wa kufanya mabadiliko kwa
sababu hata katika mataifa makubwa kama Marekani walipoona elimu yao
inaanza kutojibu matakwa ya nchi kwa wahitimu kushindwa kushindana
katika soko la ajira, Rais Ronald Regan wakati huo aliunda tume ya elimu
iliyokuja na ripoti ya ‘A Nation at Risk’,” alisema Lowassa.
Viongozi
waliohudhuria jubilee hiyo ni pamoja na Askofu Msaidizi wa Bukoba,
Methodius Kilaini, Askofu wa Jimbo la Kayanga, Mhashamu Almachius
Rwetongeza, Askofu wa Jimbo la Bukoba na mwangalizi wa Jimbo Katoliki la
Singida, Desderius Rwoma.
0 comments:
Post a Comment