SIKU
moja baada ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Mohamed Seif
Khatib kupiga marufuku pamoja na mambo mengine makada wa chama hicho
waliochukua fomu kuwania urais kushiriki midahalo, Katibu Mkuu wa chama
hicho, Abdulrahman Kinana amepinga msimamo huo.
Badala
yake, Kinana ameruhusu makada hao wanaoomba ridhaa ya kupeperusha
bendera ya chama hicho kwa nafasi ya urais kushiriki katika midahalo
iliyoandaliwa na Umoja wa Watendaji wa Kampuni binafsi (Ceo's
roundtable), huku akiwataka waandaaji wa midahalo hiyo kutenda haki ili
kuepusha mifarakano.
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini Bukoba jana, Kinana alisema midahalo hiyo
inaweza kuwafanya wananchi kuwatambua wagombea wao na kuwapima kwa hoja
kama wanaweza kuongoza nchi au la ili waweze kuwapigia kura.
“Nimepigiwa
simu na baadhi ya wagombea waliotangaza nia ya kuwania nafasi ya urais
ndani ya chama, sasa nawaambia kuwa wana hiari ya kwenda au kutokwenda
kwa sababu ni uamuzi wao binafsi na si suala la chama.
“Wakati
walipotangaza nia na kuchukua fomu walisema mengi sana ikiwamo jinsi
watakavyoweza kuongoza nchi na wananchi wamewasikia, hivyo basi chama
hakina uwezo wa kuwakataza kushiriki kwenye midahalo hiyo,” alisema.
Juzi
Seif Khatib alikaririwa na vyombo vya habari akisema hakuna mgombea
urais yeyote atakayeruhusiwa kushiriki midahalo hiyo hadi hapo chama
kitakapompata mgombea mmoja wa nafasi hiyo.
Hata
hivyo Kinana jana aliwaambia waandishi kuwa mdahalo huo si wa CCM, bali
umeandaliwa na watendaji wengine ili kuwapima wagombea hao katika
kipindi hiki wanachotaka kuwania nafasi ya uongozi.
Alisema
haoni haja ya chama kuwakataza kushiriki katika midahalo hiyo wakati
nafasi wanazozitaka ni za kitaifa na kimataifa ambazo zinawahusisha
wananchi wenyewe, hivyo wanapaswa kushiriki ili waweze kupimwa.
“Chama
hakiwezi kuwazuia watangaza nia kushiriki kwenye midahalo kwa sababu
nafasi wanazoomba ni za kuwatumikia wananchi, kama kuna mdahalo ambao
utawafanya kujibu hoja na kutoa ufafanuzi, wanachama wa CCM watawapima
hoja zao na wananchi watawapima zaidi ili waweze kujua nani anayewafaa,”
alisema.
Alisema
kutokana na hali hiyo, walioandaa midahalo hiyo wanapaswa kutenda haki
na si kuwabeba watangaza nia, jambo ambalo linaweza kuleta mifarakano
isiyo na sababu.
“Lengo la midahalo iwe ni kuwasaidia wananchi kuwafahamu wagombea wao ili waweze kufanya uamuzi sahihi,” alisema.
Alisema
kutokana na hali hiyo waandaaji wanapaswa kuangalia masilahi ya
wananchi ili waweze kujua sera zao na kujenga hoja ambazo zitawasaidia
kuwapima.
Kinana
alisema midahalo hiyo isijenge chuki na kuleta mifarakano ambayo
itawafanya wagombea kugombana, jambo ambalo linaweza kusababisha
mifarakano.
0 comments:
Post a Comment