Pages

Ads 468x60px

Friday, June 12, 2015

Godbless Lema Asikitika Uandikishaji Kuahirishwa Jijini Arusha>>



MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema amesema uandikishaji wapigakura katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, uliokuwa uanze jana na kuahirishwa, umewasikitisha kama chama kwa kuwa wananchi hawakupewa taarifa za usitishwaji wa uandikishaji huo.
 
Licha ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu kusitishwa huko, wananchi walijitokeza jana kwenye vituo vyao kwa ajili ya kujiandikisha.
 
Lema alisema hayo jana jijini Arusha wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kulalamika kuwa wananchi hawajaelezwa sababu ya kuahirishwa kwa uandikishaji huo, ambao awali ulikuwa ufanyike Juni 12 na kutangazwa tena kuwa utafanyika Juni 9 na juzi NEC ilitangaza kuwa utafanyika Juni 15 mwaka huu.
 
Alisema NEC wameahirishwa bila kutoa taarifa kwa viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa, ambao walijipanga vyema kuhakikisha zoezi hilo linafanyika na wananchi wanajiandikisha ili waweze kuwa na vitambulisho hivyo kwa ajili ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
 
“Kuahirishwa kwa zoezi hili ni hujuma zinazofanywa na NEC, maana wametangaza kuahirisha zoezi wakati wananchi leo walikuwa wamejitokeza katika vituo vilivyopangwa kuanza zoezi hili la uandikishaji, lakini tunasema hizi ni hujuma za makusudi za kuhakikisha wannachi hawaandikishwi, lakini na sisi tunasema tutaendelea na uhamasishaji wa kuajiandikisha kwa wananchi ili tarehe hiyo nyingine wajitokeze kwa wingi.
 
"Pia, ingawa kuna ongezeko la idadi ya kata za jiji hilo, ongezeko hilo si kigezo cha kuahirisha uandikishwaji, lakini na sisi tutaendelea na kampeni zetu za kata kwa kata, kuhamasisha uandikishaji hadi zoezi hilo litakapoanza la uandikishwaji kwa mfumo wa BVR."
 
Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Arusha, Richard Kitwega aliomba radhi kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha, kutokana na tume kusitisha zoezi hilo na kutaja sababu zilizofanya uandikishwaji huo kutofanyika jana kuwa ni ongezeko la kata, vifaa vya kuandikisha kutokamilika ikiwemo wino na kuahidi kuwa zoezi hilo litafanyika Juni 15 mwaka huu.
 
Awali, juzi Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Juma Idd alisema zoezi hilo lilitakiwa kuanza jana kwa kata sita na baada ya siku saba zoezi hilo litaendelea katika kata nyingine za jiji la Arusha.

0 comments:

Post a Comment

SHARE