Pages

Ads 468x60px

Friday, June 12, 2015

Wahitimu wa afya 400 kwenda hospitali za rufaa...>>>>



SERIKALI ina mpango wa kuwapeleka wahitimu wa sekta ya afya wapatao 400 katika hospitali  rufaa nchini.
 
Taarifa hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Stephen Kebwe wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Diana Chilolo (CCM).
 
Katika swali lake, Chilolo aliitaka Serikali kupelekea madaktari katika hospitali ya Ikungi kwa kuwa licha ya kupandishwa hadhi kuwa hospitali ya rufaa lakini haina wataalamu wa kutosha.
 
Dk. Kebwe alisema katika mpango wa Serikali wa kuimarisha hospitali za rufaa za wilaya, mikoa na kanda kwa sasa inao wataalamu zaidi ya 400 walio vyuoni na kwamba kwa kadri watakavyokuwa wanahitimu watapelekwa katika hospitali hizo.
 
Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Dk. Pudenciana Kikwembe (CCM), Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais, Utumishi, Celina Kombani alisema Wilaya ya Mlele ilipewa maelekezo ya jinsi ya kufanya ili kituo cha afya Iyonga kipandishwe hadhi kuwa hospitali ya wilaya.
 
“Melekezo hayo ni pamoja na kuwa na jengo la upasuaji, jengo la kuhifadhi maiti, chomeo taka, jengo la maabara, chumba cha mionzi, kuweka mfumo wa maji safi na maji taka na kufunga mfumo wa umeme kwenye majengo yote ya kituo cha afya,” alisema.
 
Kombani alisema Halmashauri ya Wilaya ya Mlele imeanza utekelezaji kwa kuingia mkataba na SUMA JKT wa Sh.bilioni 1.6  kuondoa upungufu huo.
 
Alisema inatarajiwa ifikapo Septemba, 2015 majengo hayo yatakuwa yamekamilika.
 
Katika swali lake, Dk.Kikwembe alitaka kujua lini kituo cha afya Iyonga kitapandisha hadhi na kuwa Hospitali ya Wilaya ya Mlele.

0 comments:

Post a Comment

SHARE