Uongozi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), umesema utawafukuza kazi askari wote watakaojihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu ikiwamo kuwapiga raia wanaokosana nao mitaani.
Mkuu wa Utumishi jeshini, Meja Jenerali Vicent
Mritaba alitoa onyo hilo mjibi hapa juzi alipokuwa akifunga mafunzo ya
awali ya askari wapya katika kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa la Oljoro.
“Jeshi halitawavumilia askari wanaovunja sheria
kwa kushiriki vitendo vinavyokiuka maadili ikiwamo kujichukulia sheria
mkononi,” alisema Meja Jenerali Mritaba.
Alisema jukumu la JWTZ ni kulinda mipaka ya nchi,
raia na mali zao na kushiriki kazi za kijamii kulingana na mahitaji ya
wakati huo.
Pia aliwaonya askari kutoshiriki wala kujihusisha
na makundi maovu kwa sababu itawaondolea sifa ya kuendelea kutumikia
jeshi hilo lililoundwa rasmi mwaka 1964, baada ya kuvunjwa jeshi
lililorithiwa kutoka kwa wakoloni.
Katika hatua nyingine, Meja Jenerali Mritaba
aliwataka wanajeshi wajiepushe na vitendo vinavyoweza kuwasababishia
maambuziki ya virusi vya Ukimwi.
“Mlipojiunga jeshini wote mlipimwa afya zenu na
kugundulika kuwa mpo salama. Epukeni ngono kwa sababu mkipata maambukizi
hayo ndoto zenu za kulitumikia taifa zitakatika lakini pia malengo yenu
ya kimaisha yatafifia,” alisema.
Awali, Mkuu wa Mafunzo ya Awali ya kijeshi katika
Chuo cha Kihangaiko mkoani Pwani, Kanali Ramadhani Churi alisema licha
ya changamoto kadhaa kiutawala, wahitimu hao wamefaulu katika hatua zote
mbili za mafunzo kuanzia ya wiki sita ya kuwaondoa kwenye hali ya
kawaida kuwa wanajeshi.
Kanali Churi alisema askari hao walifundishwa
uvumilivu na kuishi katika mazingira magumu ikiwamo kutolala kwa wiki
sita mfululizo, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo kisaikolojia wa
kuhimili jambo lolote gumu kwenye uwanja wa vita na mapambano.
Kaimu Kamanda wa Kikosi cha 833KJ Oljoro, Luteni
Kanali Sijaona Myala alitaja baadhi ya mambo yaliyofanikisha mafunzo
hayo kuwa ni kila mtu kuzingatia taaluma na kutekeleza wajibu wake
kuanzia kwa wakufunzi, madaktari na viongozi.
0 comments:
Post a Comment