MGOMBEA Urais wa Tanzania ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi
Amina Salum Ali amesema wanawake hawana sifa ya ufisadi na ufujaji wa
mali za umma na kwamba Tanzania inahitaji Rais Mwanamke.
Akizungumza na waandishi wa habari pembezoni mwa uwanja wa ndege wa
Karume kisiwani Pemba, Balozi Amina alisema kwamba wanawake ni watu
wanaaminifu wanaojali dhamana zao.
“Wanawake sio wafujaji, ni watu waaminifu ambao wanajali dhamana walizopewa na ni walezi wazuri” alisema Balozi Amina.
Balozi Amina alisema kwamba kazi ya Urais, inahitaji mtu mwadilifu,
mchakapazi mbali ya sifa nyingine, ambazo kama Tanzania itaongozwa na
Rais mwanamke itasonga mbele kiuchumi kwa mwendo wa haraka zaidi.
Alisema katika nchi ambazo viongozi wake ni wanawake, zimepata
mafanikio ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Alitoa mfano, Kansela wa
Ujerumani, Angela Merkel ambaye anaiongoza Ujerumani katika uchumi imara
miongoni mwa nchi za Umoja wa Ulaya (EU).
Balozi Amina anamtaja Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, marehemu
Margaret Thatcher ambaye amejenga msingi imara wa uchumi wa Uingereza
huku akimtaja pia Rais wa Brazil, Dilma Rousseff kuwa ni kiongozi mwenye
mafanikio katika nchi yake.
Balozi Amina anamtaja pia Waziri Mkuu wa zamani wa India, Indira
Gandhi kuwa naye alikuwa kiongozi hodari, shupavu na kwa uchapaji wake
wa kazi, India imesonga mbele kiuchumi kwa kuweka misingi madhubuti
wakati wa uongozi wake.
Wanasiasa wengine wanawake aliowataja ni pamoja na Waziri Mkuu wa
zamani wa Pakistan, Benazir Bhutto na Rais Ellen Johnson wa Liberia
ambaye amefanikiwa kutokomeza maradhi ya ebola kwa ushupavu wake.
0 comments:
Post a Comment