LICHA ya idadi kubwa ya makada wa CCM waliojitokeza na wanaoendelea kujitokeza kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuwania urais kupitia chama hicho tawala, Rais Jakaya Kikwete anayemaliza muda wake amesema hana mgombea, hivyo asihusishwe nao.
Amesema baadhi wamekuwa wakiomba ridhaa yake, lakini hakuna
aliyemkatisha tamaa huku akimtakia kila la heri anayejiona ana ubavu wa
kutaka kumrithi baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Aidha, amesisitiza ana imani na chama anachokiongoza, kitafanya
chaguo sahihi na mgombea wa urais atakayepeperusha vyema bendera ya CCM
katika mchakato wa kumpata Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania baadaye
mwaka huu.
Rais Kikwete alisema hayo juzi usiku katika mkutano wake na Jumuiya
ya Watanzania waishio Uholanzi, uliofanyika katika hoteli ya Crownie
Plaza mjini hapa.
Alisema hayo alipokuwa anaelezea hali ya kisiasa nchini na pia
maandalizi yanayoendelea ya uchaguzi mkuu ujao na pia mchakato wa Kura
za Maoni ya Katiba Inayopendekezwa.
Hana mgombea
Akizungumzia mbio za urais zinazoendelea kushika kasi, alisema hali
ya kisiasa ya Tanzania ni shwari, licha ya kuwa kumekuwa na kishindo
katika kuwania kumrithi.
“Nyumbani hali ni shwari, lakini kwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi
kuna mengi yanayoendelea, hasa mchakato wa kuwania Urais… huko CCM mpaka
leo (juzi) watu 15 walishachukua fomu, na wengine zaidi ya 15 ama
wametangaza nia au wanakusudia kufanya hivyo.
“Ndiyo demokrasia ndani ya
CCM, lakini niwahakikishie acheni waumane, lakini mimi binafsi sina
chaguo langu. Chama ndicho kitakachoamua na ninaamini kitatupatia
kiongozi sahihi kwa saizi na hadhi ya CCM na huyu atatuvusha mpaka
Ikulu,” alisema.
Aidha, alisema wapo wanaojipitisha kwake wakiomba kuungwa mkono,
lakini pamoja na hayo, akasisitiza hana mgombea.
“Jana (Jumapili), kuna
mtu alinitumia ujumbe akisema anakusudia kutia nia hivyo nimpe baraka
zangu…nikamwambia `Goodluck’ (Kila la heri), sasa kama alitafsiri ndiyo
tayari mambo safi, aah…sijui bwana, ila mimi sina mgombea.
“Nasisitiza
chama chetu ni makini na kitatupatia mgombea makini. Mwenyezi Mungu
atuepushie mbali ili tusipate kiongozi atakayeipeleka nchi pabaya,”
alisema na kuwataka Watanzania hao kutokuwa na hofu juu ya mchakato huo
ndani ya CCM.
0 comments:
Post a Comment