WAZIRI wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira amesema iwapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitafanya kosa kumsimamisha mgombea mla rushwa, kitapoteza dola.
Akizungumza jana na waandishi wa habari baada ya kudhaminiwa katika
ofisi za CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Wassira alisema kamwe wana CCM
hawatakubali kupoteza dola, badala yake atateuliwa mtu safi.
Mgombea huyo alisema Watanzania hawana nchi, ambayo iko sokoni na
akaongeza kuwa kama Tanzania ingekuwa inauzwa, wangetangaza zabuni ya
kuinunua, hivyo akawataka wagombea wenzake wanaotumia rushwa, kuacha.
Alisema yeye hatoi rushwa na anatafuta wadhamini mikoani kwa kutumia gari na sio kupanda ndege au helikopita.
Alisema hadi jana alikuwa ameshapata wadhamini kutoka mikoa 15 na
akasisitiza kuwa atazunguka nchi nzima, kusaka wadhamini kwa kutumia
gari lake.
Hata hivyo, Wassira aliwasihi wagombea urais wa CCM ambao wametangaza
nia na wale ambao wamechukua fomu kuomba kugombea urais, wasigombane
kwani kufanya hivyo kutawanufaisha wapinzani.
Alisema ugomvi wa miongoni mwa wana CCM, uliwanufaisha wapinzani
katika majimbo ya Kawe na Ubungo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010,
hali ambayo ilisababisha CCM kupoteza majimbo hayo kwa vile tu wagombea
waliingia kwenye ugomvi.
“Mimi nagombea na sitaki kugombana na mtu na nawasihi wenzangu
wengine pia tusiingie kwenye ugomvi kwani kufanya hivyo wapinzani
watapita katikati yetu na kushinda uchaguzi,” alisema Wassira.
Wassira alisema ana hakika atashinda na atakipokea kijiti kutoka kwa
Rais Jakaya Kikwete na akawataka wana CCM, waamua kwa haki na sio kwa
rushwa.
“Haki itapatikana katika mazingira tulivu na sio mazingira ya rushwa,” alisema Wassira.
“Haki itapatikana katika mazingira tulivu na sio mazingira ya rushwa,” alisema Wassira.
0 comments:
Post a Comment