MBUNGE
wa Viti Maalumu, Christowaja Mtinda (Chadema),ameitaka Serikali
kuufanyia utafiti mmea wa bangi ili kubaini iwapo unaweza kutumika kama
dawa ya kutibu magonjwa ya binadamu.
Akiuliza
swali la nyongeza bungeni jana Mtinda alisema iko mikoa ambayo bangi
huota yenyewe kama vile Njombe, Iringa na Mara na kwamba wakazi ya mikoa
hiyo huitumia kama chakula.
“Sasa ni utafiti gani ambao Serikali imeufanya kubaini iwapo mmea wa bangi unaweza kutumika kama dawa?” alihoji.
Aidha,
aliitaka Serikali kutoa elimu kwa wananchi ambao wanaamini kwamba
matumizi ya bangi yanaimarisha afya na kuongeza nguvu za kufanya kazi.
Akijibu
swali hilo, Naibu Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma
Nkamia alisema hakuna utafiti wowote utakaofanyika kwa mmea wa bangi kwa
kuwa ni haramu na ni kinyume cha sheria.
“Serikali
inasisitiza bangi ni haramu na matumizi yake ni kinyume na sheria hata
kama bangi hiyo itakuwa imeota yenyewe, madhara ya bangi kwa nchi ni
makubwa,” alisema.
Alisema pia hakuna utafiti ulioonyesha kwamba bangi inaongeza nguvu za aina yoyote ile.
Awali
akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Leticia Nyerere
(Chadema), Nkamia alisema Washington DC ni jimbo la tatu kupitisha
matumizi ya bangi kama dawa kwa wagonjwa wenye maumivu sugu pamoja na
kuliwaza watu walioumia katika ajali.
“Sheria
hiyo ilianzia Jimbo la Alaska na Colorado ambao walishapitisha sheria
hizo kwa matumizi ya kipimo kisichozidi gramu 56 kwa mtumiaji mwenye
umri kati ya miaka 21 na kuendelea.
“Halikadhalika
mtumiaji hapaswi kuvuta mbele ya kadamnasi, kuuza wala kusafirisha na
akifanya hivyo ni kosa la jinai na hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi
yake,” alisema.
Alisema
msimamo wa Serikali ya Tanzania ni kwamba inafuata sheria ambayo
inaeleza kwa kina kuwa mtu yoyote atakayejihusisha na kutumia,
kuhamasisha matumizi,kuuza, kusafirisha, kuhifadhi na kujihusisha kwa
namna yoyote ile na bangi ni kosa la jinai.
Alisema
adhabu kwa makosa hayo hufikia hadi kifungo cha maisha. Katika swali
lake Nyerere alitaka kujua msimamo wa Serikali kuhusu kuhalalishwa kwa
matumizi ya bangi kwa Serikali ya Washing DC Marekani.
0 comments:
Post a Comment