Ofisi
ya Bunge imebaini uwepo wa Waraka usiokuwa na Nambari ya Kumbukumbu
wala Tarehe wenye kichwa “KUIDHINISHWA KWA MFUKO WA FOCUS VICOBA”
unaosambaa kupitia njia mbalimbali ikiwemo mitandao maarufu ya Facebook
na WhatsApp. Waraka huo una maneno yafuatayo:
“Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania linaidhinisha na kutambua uwepo wa mfuko wa utoaji mikopo FOCUS VICOBA. Viongozi wakuu wa bunge na wabunge kwa ujumla tumepitisha huduma za mikopo inayotolewa na Taasisi ya Vicoba kupitia mfuko wa FOCUS VICOBA kwa lengo la wajasiriamali kupata mikopo inayotolewa katika mfuko huu wa FOCUS VICOBA.”
Ofisi
ya Bunge inapenda kuutaarifu umma kwamba Waraka huo siyo wa kweli na
kwamba Viongozi Wakuu wa Bunge na Wabunge kwa ujumla hawajawahi
kujishughulisha na hoja wala masuala ya Taasisi ya VICOBA.
Aidha,
Ofisi ya Bunge inapenda kuueleza umma kwamba barua na nyaraka zote za
Bunge hutumia nembo ya Bunge kama inavyoonekana hapo juu na si ya
Serikali. Vile vile muhuri na sahihi ya Katibu wa Bunge viliyo katika
Waraka huo havifanani kabisa na muhuri na sahihi halisi ya Katibu wa
Bunge. Hivyo ni dhahiri kwamba Waraka unaosambaa ni wa kutunga.
Wakati
Ofisi ya Bunge inaendelea kufanya uchunguzi ili kujua Wahusika na
kutafakari dhamira ya kutungwa na kusambazwa kwa Waraka huo na kuchukua
hatua stahiki, Umma unatahadharishwa kutojihusisha na Mfuko wa FOCUS
VICOBA kwa imani ya kwamba umeidhinishwa na Bunge.
Imetolewa na:
Idara ya Habari na Elimu kwa Umma,
Ofisi ya Bunge,
DODOMA Tarehe 15 Juni 2015
0 comments:
Post a Comment