Pages

Ads 468x60px

Friday, June 19, 2015

Serikali Yawaahidi Watanzania kunywa maji ya bomba bila kuchemsha...>>>



SERIKALI  inaendelea na jitihada mbalimbali za uboreshaji wa maji safi na salama ili maji yanayotoka bombani yaweze kunywewa moja kwa moja bila kuchemsha.

Taarifa hiyo imetolewa bungeni leo na Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Maria Hewa (CCM).
 
Katika swali lake Maria Hewa alitaka kujua lini wananchi wataruhusiwa kunywa maji ya bomba moja kwa moja bila kuchemsha.
 
Makalla amesema serikali inafanya maboresho ya mitambo ya maji safi na ujenzi wa miradi mipya mijini na vijijini.
 
“Katika utekelezaji wa miradi hiyo, suala la miundombinu ya kutibu maji limepewa kipaumbele.
 
“Aidha, Serikali imeandaa mpango unaohusika na uratibu wa usafi na usalama wa maji kuanzia kwenye chanzo hadi kwa mtumiaji.
 
“Mojawapo ya matokeo ya mpango huu ni kupunguza gharama kubwa za kusafisha na kutibu maji ya kunywa.
 
“Mpango huu unahusisha taasisi zote za usambazaji wa maji ili kutoa uhakika wa maji yanayotumika kuwa ni safi na salama, hivyo jitihahada hizi zikifanyika maji ya bomba yataweza kunyweka bila kuchemshwa,” alisema.
 
Aidha, alisema majisafi na salama ni yale ambayo yanapitia hatua zote za kusafisha na kutibu, hivyo huduma ya usambazaji maji mijini inahusisha ujenzi wa miradi yenye miundombinu ya kusafisha na kutibu maji kutegemeana na aina ya chanzo na ubora wa maji hayo.
 
“Maji huhakikiwa ubora wake kabla na baada ya kusambazwa ili kuhakikisha usalama wake unakuwa endelevu, hata hivyo ushauri wa kuchemsha maji ya kunywa ni tahadhari endapo uchafuzi utajitokeza kwenye mifumo ya usambazaji,” alisema Makalla.

0 comments:

Post a Comment

SHARE