Pages

Ads 468x60px

Sunday, June 28, 2015

Wananchi wala ubuyu kutokana na njaa-Manyoni



MBUNGE wa Manyoni Mashariki, Kapteni John Chiligati, amesema baadhi ya wananchi jimboni kwake wameanza kula ubuyu kutokana na kukabiliwa na tatizo la njaa.

Katika swali lake bungeni jana, Mbunge huyo alitaka kujua ni lini Serikali itapeleka chakula cha msaada haraka ili kuwanusuru wananchi hao.

“Lini Serikali itaanza kugawa chakula cha msaada kwa kuwa jimboni kwangu kuna uhaba wa chakula, hasa katika maeneo ya Kintiku ambapo baadhi yao wameanza kula ubuyu?” alisema Kapteni Chiligati.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi, alisema taratibu za kuomba chakula cha msaada zinatakiwa kuanzia wilayani kwa kufanya tathmini.

“Wilaya ikishafanya tathmini inatakiwa kuipeleka katika kikao cha Ushauri cha Mkoa (RCC), RCC itapeleka Ofisi ya Waziri Mkuu ambao wataleta wizarani kwetu kwa ajili ya kupeleka chakula cha msaada. Chakula kipo cha kutosha, mikoa husika inatakiwa kufanya tathmini ili ituletee watu wasije wakafa njaa,” alisema.

Awali Zambi akijibu swali la msingi la Kapteni Chiligati, lililohoji iwapo serikali ipo tayari kushirikiana na wananchi wa Manyoni kupitia Halmashauri ya wilaya hiyo kuhakikisha ujenzi wa bwawa la Mbwasa unakamilika, alisema ujenzi huo utafanyika pamoja na skimu ya umwagiliaji ya Mwiboo.

“Skimu ya Mwiboo haipo katika skimu 78 zinazotekelezwa kupitia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN). Wizara kwa kushirikiana na halmashauri za wilaya zimeandaa andiko kwa ajili ya kuomba fedha kwa washirika wa maendeleo ambao maombi ya Sh milioni 400 yamewasilishwa,” alisema Zambi.

0 comments:

Post a Comment

SHARE