MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaonya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba na wenzake kwa kuchelewa na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee kwa kutohudhuria mahakamani.
Washtakiwa hao walionywa kwa nyakati tofauti jana wakati kesi zao zilipokwama kuendelea kusikilizwa kwa sababu yao.
Kesi inayomkabili Profesa Lipumba na wenzake 31 ilitakiwa kuendelea
kusikilizwa, lakini iliahirishwa kwa sababu hakimu anayeisikiliza,
Cyprian Mkeha hakuwapo na washtakiwa walichelewa kufika mahakamani.
“Mahakama inatoa onyo kwa Profesa Lipumba na wenzako 31 kwa kuchelewa
kufika mahakamani, utaratibu wa mahakama kesi zinaanza saa tatu kamili
asubuhi, mnatakiwa kuheshimu muda sababu kila mtu anaishi mbali.
“Nimewapa onyo, kesi itaendelea Julai 10 mwaka huu washtakiwa wote
mnatakiwa kuwahi,” alisema Hakimu Huruma Shahidi aliyeahirisha kesi
hiyo.
Profesa Lipumba na wenzake wanakabiliwa na mashtaka ya kufanya
maandamano bila kibali na kukaidi amri halali ya polisi iliyowataka
kutawanyika Januari 27, mwaka huu.
Wakati huo huo, mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Janeth Kaluyenda
imemuonya Mdee kwa kutohudhuria mahakamani na kwamba iwapo hatafika
Julai 6, mwaka huu itatoa hati ya kumkamata.
“Kinachoendelea ni maneno yasiyo na ushahidi, mshtakiwa hayupo na
wadhamini hawapo, tutenganishe siasa na mahakama, ifike wakati tuheshimu
mahakamani, hakuna sababu ya kuendelea na kesi kama mshtakiwa hayupo.
“Tarehe ijayo Julai 6 awepo mahakamani ili kesi iendelee kusikilizwa,
iwapo hatafika sitajali mbunge wala katibu kata, nitatoa hati ya
kumkamata,” alisema Kaluyenda.
Awali Wakili wa Serikali Mkuu, Benard Kongola akisaidiana na Joseph
Maugo, waliomba mahakama itoe hati ya kumkamata mshtakiwa kwani sababu
za kutofika mahakamani hazina msingi.
Wakili wa utetezi, Peter Kibatala akisaidiana na John Mallya walidai
Mdee anahitaji ruhusa ya Spika wa Bunge ndiyo atoke bungeni.
Mbali na Mdee, washtakiwa wengine ni Renina Leafyagila na Sophia Fanuel.
Washtakiwa wengine, Rose Moshi, Anna Linjewile, Mwanne Kassim, Edward Julius, Martha Mtiko na Beatus Mmari waliachiwa huru.
Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Oktoba 4, mwaka huu, katika Mtaa wa
Ufipa, uliopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam, isivyo halali,
washtakiwa walikiuka amri halali ya Mrakibu wa Polisi (SP), Emmanuel
Tillf iliyowataka kutawanyika.
Ilidaiwa kuwa siku na mahali lilipotokea tukio la kwanza, washtakiwa
walifanya mkusanyiko isivyo halali kwa lengo la kuandamana kwenda Ofisi
ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
0 comments:
Post a Comment