WANACHAMA watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo wanatarajiwa
kuchukua fomu, kuomba ridhaa ya uteuzi wa kuwania urais wa Tanzania,
wakati wakiwa hawajatangaza nia kama ilivyo kwa wengi wao.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mohammed Gharib
Bilal, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na Katibu Msaidizi wa Siasa
na Ushirikiano wa Kimataifa katika Ofisi Ndogo ya CCM, Dar es Salaam,
Amos Robert wanachukua fomu leo mjini hapa.
Watatu hao ambao hawajatangaza nia ya kuwania nafasi hiyo ya juu ya
uongozi wa nchi wakipitia CCM, wataungana na mawaziri wakuu wa zamani,
Frederick Sumaye, Edward Lowassa na Balozi Ali Karume kuchukua fomu leo.
Sumaye, Lowassa na Karume wote wamekwishatangaza nia ya kumrithi Rais
Kikwete, tofauti na Dk Bilal, Magufuli na Robert ambao hawajatangaza
popote nia yao.
Kwa mujibu wa Katibu wa Halmshauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) wa
Oganaizesheni, Dk Muhammed Seif Khatib, Robert atakuwa wa kwanza
kuchukua fomu leo kuanzia saa nne asubuhi katika Makao Makuu ya CCM.
Dk Khatib alisema Katibu Msaidizi huyo atafuatiwa na Sumaye saa 5:30
asubuhi, Dk Bilal atafuata saa saba kamili, Balozi Karume saa 8:30
mchana, Lowassa ambaye aliahirisha jana atafuata saa 9:30 alasiri na
Magufuli atafunga dimba kwa leo atakapochukua saa 10:30 jioni.
Lowassa aliahirisha kuchukua jana baada ya kuelezwa kuwa ilitokana na
kushiriki kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Ukonga, marehemu Eugen
Mwaiposa, ambaye aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati yake ya Mambo ya Nje ya
Bunge la Tanzania.
Dk Bilal alikuwa mmoja wa wanaCCM waliowania urais
wa Zanzibar mwaka 2010 na alishindwa na Rais Dk Ali Mohammed Shein
katika uteuzi wa CCM.
Rais Kikwete baadaye alimpendekeza kuwa Mgombea Mwenza na aliposhinda
awamu yake hiyo ya pili kuiongoza nchini, akawa Makamu wa Rais.
Dk Magufuli amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa wanaCCM wanaofaa kwa urais
wa Tanzania, na hajawahi kutangaza nia yake, ingawa vyombo vya habari
vimekuwa vikimtaja kuwa miongoni mwa wanaofikiria nafasi hiyo.
Awali jana, wagombea wanne waliokwisha kutangaza nia, walifungua pazia
la uchukuaji fomu za uteuzi wa CCM ambazo zitatolewa hadi Julai 2,
mwaka huu.
Wa kwanza aliyekabidhiwa fomu na Dk Khatib alikuwa Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya akifuatiwa na
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wassira, Balozi wa Umoja
wa Afrika (AU) Marekani, Amina Salum Ali na Mbunge wa Bunge la Afrika
Mashariki, Charles Makongoro Nyerere.
Profesa Mwandosya akifuatana na mkewe Lucy, aliwaambia waandishi wa
habari kuwa baada ya kushika nafasi ya tatu nyuma ya Rais Kikwete na Dk
Salim Ahmed Salim mwaka 2005, anaamini sasa zamu ni yake.
“Uamuzi wa kuchukua fomu ni uamuzi mzito sana, inabidi ujiandae
kisaikolojia kwa maana ya kiakili, kiafya, kimaono, dhamira na dhima.
Lakini kubwa zaidi huwezi kuwa na kiburi kama hutokani na wananchi
wenyewe au huwawakilishi, kwa hiyo ni dhima kubwa,” alisema.
Profesa Mwandosya aliongeza, “Chimwaga nilikuwa wa tatu, huko sio
kushindwa. Nikasema nimepata shaba si haba, sasa yule wa pili hayupo,
kwa hiyo, naamini ni wakati wa kupata dhahabu. Ofisi yangu sasa iko ghorofa ya chini, ninachoomba ni kupanda ngazi.”
Kwa upande wake, Wassira naye akifuatana na mkewe, alisema uzoefu wa
muda mrefu serikalini pamoja na uchapakazi na uadilifu wake, ni miongoni
mwa sababu zinazomfanya aombe ridhaa ya uteuzi huo.
“Kwa hiyo, naomba nianze safari, siyo safari kama ile nyingine, hii
ni safari ya uhakika ya kutafuta fursa, kwa nia, kwa uwezo, na sababu
ninao uzoefu, hili sio jambo la bahati mbaya. Nimeandaliwa na niko tayari,” alisema.
Balozi Amina akifuatana na
waliowahi kuwa viongozi wenzake wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Anna
Abdallah na Halima Mamuya, alisema atajenga uchumi imara wa kuiwezesha
Tanzania ijitegemee.
Alisema chini ya kaulimbiu yake ya ‘Matumaini Mapya kwa Kizazi
Kipya,’ atazingatia mambo makuu matatu ambayo ni kuongeza kasi ya ukuaji
wa uchumi kwa kupanga upya vipaumbele vya maendeleo kwa kutumia vizuri
rasilimali za nchi ili ziwanufaishe wananchi.
Alisema anayo nia thabiti, uwezo na uzoefu wa kutosha kuizusha
Tanzania kutoka ilipo sasa, huku akiahidi kuanzisha Mahakama Maalumu ya
kushughulikia rushwa kwani alikiri ni rushwa na ufisadi ni tatizo kubwa
sasa.
Kuhusu kama Tanzania iko tayari kwa Rais mwanamke, alisema, “takwimu
zinaonesha kuwa nusu ya Watanzania ni wanawake, na kwa sababu hiyo,
wanao uwezo wa kutoa rais.Lakini kubwa wanawake ni waadilifu na waaminifu, wanao uwezo wa
kupambana na rushwa na ufisadi, na hata katika matukio haya, ni nadra
kuwakuta.”
Aliyefunga pazia jana alikuwa Charles Makongoro Nyerere, ambaye ni
mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na sasa Mbunge wa Bunge la
Afrika Mashariki.
Makongoro alizungumzia kwa kirefu rushwa ilivyo tatizo sasa ndani ya
CCM na kutaka zichukuliwe hatua kukabiliana na tatizo hilo haraka
iwezekanavyo.
“Rushwa ikitawala katika chama ni hatari sana, kwani kwa kuwa kina
uhusiano na serikali, basi hata huko hali itakuwa mbaya. Rushwa inaleta
heshima mbaya.
“Mwenyekiti wetu wa CCM, Rais Kikwete amewaambia waache rushwa,
lakini hawaachi. Rais wetu siyo dhaifu, ila mstaarabu na mwenye huruma,
lakini wanamuangusha sana.Nasema turudishieni chama chetu,” alisema.
Makongoro aliyewahi kuwa
Mwenyekiti wa zamani wa Mkoa wa Mara, alifuatana na wazee tisa kutoka
Zanzibar, na kueleza kuwa mdhamini wake wa kwanza Zanzibar atakuwa Rais
wa Awamu ya Tano, Salmin Amour Juma maarufu kwa jina la Komandoo.
Baada ya kukabidhiwa fomu hizo, wagombea hao walianza kusaka saini za
wadhamini 450 katika mikoa 15 ya Tanzania Bara na mikoa mitatu ya
Tanzania Zanzibar, ikiwamo ya Unguja na Pemba.
Wakati huo huo, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja atatangaza nia
ya kugombea urais katika ukumbi wa Benki Kuu (BoT) mjini Mwanza leo saa tano asubuhi.
0 comments:
Post a Comment